23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Werema atangaza mkakati mbadala Katiba Mpya

Frederick Werema
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema

NA AGATHA CHARLES

OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imevunja ukimya tangu kuanza kwa awamu ya pili ya Bunge Maalumu la Katiba na kutangaza mkakati mbadala endapo Bunge hilo litashindwa kupata Katiba Mpya.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, alitangaza mkakati huo jana katika mkutano na waandishi wa habari katika Ukumbi wa Haki na Utawala Bora jijini Dar es Salaam.

Jaji Werema alikuwa akizungumzia hatima ya upatikanaji wa Katiba Mpya na mwenendo wa vikao vya kamati za Bunge Maalumu vinavyoendelea sasa huko Dodoma, ambavyo vimesusiwa na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Alisema tathmini iliyofanyika ya mwenendo wa vikao hivyo, imeonyesha kuwa theluthi mbili inayohitajika ili kupitisha vifungu vinavyojadiliwa inapatikana isipokuwa wasiwasi umebaki kwenye kupitisha vifungu hivyo wakati wa vikao vya pamoja vya wabunge wote.

Jaji Werema alisema kwa kutambua hilo, iwapo akidi ya theluthi mbili ya wajumbe haitapatikana wakati wa kupitisha Katiba iliyopendekezwa, baadhi ya vifungu vitakavyopitishwa vitachukuliwa na kupelekewa kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kuingizwa kwenye Katiba ya sasa ya mwaka 1977.

“Kwa sasa akidi kwenye kamati inatosha, tukifikia Bunge kuja na Katiba inayopendekezwa na kama hakuna theluthi mbili tutarudi kwenye Bunge la kawaida (Bunge la Jamhuri ya Muungano) na kukubaliana, yaliyokuwa hayana ubishi tutayaweka na kuyatumia kwenye Katiba ya sasa, likiwamo suala la mgombea binafsi,” alisema Jaji Werema.

Akizungumzia utata uliojitokeza kwenye sura ya kwanza na sita, alisema siyo za muhimu katika rasimu, bali kuna maeneo mengi likiwamo suala la adhabu ya kifo ambalo amekuwa akiliomba lifutwe ingawa wengi wanapinga.

Jaji Werema alisema suala la maridhiano ni la kidemokrasia na lazima lifanyike ingawa wasuluhishi watakuwa wananchi kutokana na Bunge hilo kuwa na kazi tatu tu ikiwamo kujadili rasimu, kutoa Katiba na kutunga masharti ya mpito.

“Sheria inasema Bunge litapokea rasimu na kuijadili na kuja na Katiba iliyopendekezwa na kuipeleka kwa wananchi watakaoipigia kura,” alisema Jaji Werema.

Pamoja na hayo, aliwataka wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba kuwa wavumilivu kwa kukaa kimya hasa wanapokosolewa.

“Wazee wangu wamefanya kazi kubwa, wapo wanaowabeza na wao wanarudisha majibu, mimi nashauri wabaki washauri, kuna mmoja maji yalimfika shingoni kwenye mdahalo, wavumilie, ukijibu ni kidogo, huko nyuma mwaka 1965 Kawawa aliongoza kupata Katiba, akaja Thabit Kombo na baadaye Mwakawago, kulikuwa na hali kama hii, lakini walitulia na maridhiano yalifanyika,” alisema Jaji Werema.

Mbali na kutangaza mkakati huo mpya, Werema alieleza tamaa aliyonayo moyoni kuhusu uwepo wa Mbunge wa Singida Mashairiki, Tundu Lissu (Chadema) katika Bunge hilo.

Alisema katika Bunge la Katiba anamtamani mwanasheria mwenzake Lissu kwa sababu anaweza kuwa na mchango mzuri katika kipengele cha haki za binadamu.

“Ningependa kusikia sauti ya Lissu kuhusu haki za binadamu na si yeye kuwa Kibandamaiti kwenye maandamano, mawakili wengine wanaendelea kujadili, hasa suala la adhabu ya kifo, iwepo rekodi yao kuwa kulikuwa na watu wanapinga adhabu hiyo. Pia sheria hairuhusu maandamano ili Bunge livunjwe,” alisema Jaji Werema.

Alirejea kusisitiza wito uliokwishatolewa na viongozi mbalimbali na wananchi wengine kuwa wajumbe wa Ukawa wanapaswa kurudi bungeni kuendelea kuwawakilisha wananchi, na alimtaja pia Maria Sarungi ambaye ni mjumbe kutoka kundi la 201 kuwa mmoja wa watu muhimu wanaokosekana ndani ya Bunge hilo.

“Kusitisha tunaweza tukakubaliana kwa hilo, lakini si kuvunja, nimekutana na Ukawa kimya kimya wakati mwingine nyumbani kwangu Dodoma ama kwenye mtandao, na nimefanya hivyo kwa kuwa mimi mwanasheria msuluhishi.

“Kwa mfumo wa sheria uliopo sasa hakuna kifungu chochote kinachotoa mamlaka kwa rais kulivunja Bunge, hivyo akifanya hilo atakuwa anavunja Katiba aliyoapa kuilinda,” alisema Jaji Werema.

Alisema kundi la Ukawa kabla halijatoka bungeni lilikuwa limekwishajadili kipengele cha kwanza kinachohusu masuala ya mipaka na cha sita cha muundo wa Muungano, hivyo wakirudi wataendelea na eneo jingine.

Tangu mwezi Aprili mwaka huu, wajumbe wa vyama vitatu vya upinzani vinavyounda Ukawa, ambavyo ni Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF wamekuwa nje ya Bunge la Katiba kwa madai ya kutoridhika na mwenendo wake.

Tayari viongozi mbalimbali akiwamo Msajili  wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, walijitokeza kutafuta suluhu kwa kuwakutanisha Ukawa na CCM kwa nia ya kupata mwafaka kwa kuwataka warudi bungeni, lakini jitihada zao hazikuzaa matunda kwani wamekuwa wakisisitiza kutorudi.

Kabla ya kumalizika kwa mkutano huo, Jaji Werema alisema anatarajia kuzungumzia masuala mbalimbali siku chache zijazo likiwamo suala la Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na mgogoro wake na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles