NA MWANDISHI WETU, BUNDA
MKURUGENZI wa Shirika la Kivulini, Ally Yassin ameiomba Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kutoa mwongozo kwa wenyeviti wa mitaa na vijijini kuhusu tozo zinazopaswa kutolewa na wananchi wanapopata huduma za kiserikali kwa wenyeviti hao.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Bunda mkoani Mara katika mafunzo ya kuwajengea uwezo wenyeviti wa serikali za mitaa na vijiji kuhusu majukumu yao katika ulinzi na usalama wa jamii, Yassin alisema yapo madai ya wananchi kutozwa fedha wanapohitaji huduma kwa wenyeviti hao.
Yassin aliyekuwa akiangazia juu ya vitendo vya ukatili na manyanyaso wanayopata akina mama na watoto katika jamii alisema wahanga wa matukio hayo hawajapata kushughulikiwa kikamilifu katika ngazi za mitaa na vijiji na kufanya vitendo hivi kuendelea kushamiri ndani ya jamii.
Alisema wapo baadhi wanaodai kutozwa fedha katika ngazi hizo ili kupata usaidizi na wakati mwingine kufanya maelewano katika ngazi za mitaa na vijiji bila wahanga kupata haki zao na watuhumiwa kufichwa bila kufikishwa mahakamani.
“Tunahitaji wenyeviti hawa wajue michango yao katika kushughulikia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kama kuna tozo yoyote basi iwekwe wazi katika mwongozo wa serikali”Alisema Yassin.
“sisi tunajua kuwa huduma hizi zinatolewa bure hivyo wenyeviti wazisimamie katika kuhakikisha kuwa wahanga wanatendewa haki na kukomesha vitendo hivi ndani ya jamii” alifafanua.
Aidha aliiomba Tamisemi kushughulikia changamoto zinaziwakabili wenyeviti hao katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na stahiki zao kama posho, vifaa vya kazi na zinginezo ili kuwawezesha kufanya majukumu yao inavyotakiwa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili aliwataka wenyeviti hao kutenda majukumu yao kama viongozi wa serikali badala ya kuwaacha wananchi kwenda kutafuta suluhu ya matatizo yao katika ngazi za wilaya na mikoa na wakati mwingine kufikisha kwa Rais.
Bupilipili alisema si haki wananchi kupata usumbufu kwenda mwendo mrefu kutafuta suluhu wakati wenyeviti wao wako karibu nao na kwamba kero zao zinapaswa kushughulikiwa hatua kwa hatua.
Aliwataka wasimamie ulinzi na usalama wa wananchi wakati huu wauchaguzi huku wakihimiza wananchi kufanyakazi kwa bidii kwa kuwa kuna maisha zaidi baada ya uchaguzi.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wenyeviti hao kuacha kuwa miungu watu nakuwatisha wananchi wanapotatua kero za wananchi huku akiwataka wawe mifano bora kwa jamii kuanzia wanavyosimamia familia zao wenyewe.