27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WENYEVITI SERIKALI ZA MITAA WAGOMA KUGEUZWA NYOKA WA KIBISA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, George Simbachawene
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, George Simbachawene

Na Dennis Luambano, Dar es Salaam

KISA na mkasa wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kunyang’anywa mihuri yao kilianza kuibuka Nyamagana jijini Mwanza.

Kisa hicho kilianza taratibu Oktoba, mwaka jana pale wenyeviti 174 wilayani humo walipoambiwa wairudishe mihuri hiyo kwa watendaji wao wa mitaa.

Wao waligoma kwa hoja kwamba watashindwa kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi waliowachagua kwa kuwa Mwanza yote kwa ujumla wake ina upungufu wa zaidi ya maofisa watendaji 100 wa mitaa.

Wenyeviti hao walienda mbali zaidi kugomea agizo la kunyang’anywa mihuri kwa kutoka nje ya mkutano ulioitishwa wakati huo na Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Mary Tesha.

Licha ya kasi ya wenyeviti wa Nyamagana kugomea agizo hilo kuwa kubwa, lakini katika baadhi ya mikoa nako likataka kuanza kutekelezwa huku Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikikaa kimya kana kwamba hawakusikia juu ya malalamiko hayo.

Si hivyo tu, pia wenyeviti wa Jiji la Dar es Salaam hasa katika manispaa za Kinondoni na Temeke, waliandikiwa barua ya kurudisha mihuri hiyo kwa watendaji wao na kuanza kupinga, kwa mara nyingine Tamisemi ilikaa kimya.

Barua hizo walianza kuandikiwa mwanzoni mwa Januari, mwaka huu huku nakala zikipelekwa kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa manispaa za Kinondoni na Temeke, madiwani wa kata husika, polisi na maofisa watendaji wa mitaa.

Baada ya wenyeviti hao kuandikiwa barua za kutekeleza agizo la kurudisha mihuri wakaanza kupaza sauti za kupinga.

Walianza kama masihara, kwanza kwa kutishia kujiuzulu nyadhifa zao kama Serikali itaendelea na msimamo wake wa kuwanyang’anya mihuri ambayo kwao ni vitendea kazi vyao.

Pili wakamwomba Waziri wa Tamisemi, George Simbachawene, kutoa kauli kuhusu agizo la wao kunyang’anywa mihuri.

Pia wakaweka msimamo kwa kutoa saa 24 kwa Katibu Mkuu Tamisemi, Mussa Iyombe, kuwaomba radhi kutokana na barua ya agizo hilo aliyoiandika Novemba 30, mwaka jana kwenda kwa wakurugenzi wa manispaa zilizopo Tanzania Bara.

Hawakuishia hapo, bali walitangaza kususia shughuli za maendeleo katika mitaa yao ikiwamo kufichua wahalifu.

Mwenyekiti wa wenyeviti wa Manispaa ya Kinondoni, Juma Uloleulole, alisema na kuongeza: “Tunatoa siku saba kwa wakurugenzi wote walioandika barua kwa watendaji wa kata na Jeshi la Polisi kuwataka watupokonye mihuri watuombe radhi. Wakikaidi maazimo yetu tutajiuzulu nchi nzima na uchaguzi uandaliwe upya.”

Baada ya wenyeviti hao kujenga hoja zao na kutishia kwenda mahakamani ndipo Simbachawene alipokutana nao mapema wiki hii na kutoa tamko la kusitisha mwongozo wa Novemba, mwaka jana uliowataka wenyeviti wa Serikali za mitaa na vijiji kurudisha mihuri, hadi utaratibu mzuri wa utekelezaji wake utakapopangwa.

Simbachawene anasema kusitishwa kwa mwongozo huo kumetokana na baadhi ya wenyeviti kulichukulia agizo hilo kama hujuma za kutaka kupokwa madaraka waliyonayo katika maeneo yao.

“Nasitisha mwongozo uliotolewa hadi tutakaposhirikiana na wahusika kuona namna bora ya kuutumia, lakini wahusika wanapaswa kufahamu kwamba hatukuwa na nia mbaya bali lengo lilikuwa ni kuwabana wenyeviti wasio waaminifu,” alisema na kuongeza:

“Suala hili limetuletea madhara makubwa kwa ngazi ya Serikali za Mitaa hadi kuna watu wametangaza kwenda mahakamani kuhoji hatua hii na wengine wanaendelea kufanya mikutano katika maeneo yao.

“Kwa hali hiyo nafuta mwongozo huu ili wenyeviti muendelee kuwa na mihuri hadi tutakaposhirikiana kuona namna bora ya kutumia agizo hili.”

Pia, anasema Serikali iliamua kuweka mwongozo huo kwa lengo la kupunguza migogoro mbalimbali inayojitokeza hasa ya ardhi inayotokana na wenyeviti wanaotumia mihuri hiyo kumilikisha watu maeneo kinyume cha sheria.

“Tumefika hapa kwa sababu ya mazoea tuliyonayo, baadhi ya wenyeviti wamekuwa wakitembea na mihuri mifukoni na kuwagongea watu kuwatambulisha hata wasio husika na kuuza viwanja vya Serikali jambo ambalo si sawa,” anasema.

Aidha, anasema wenyeviti wa Serikali za Mitaa si lazima kumiliki muhuri kisheria kwa mujibu wa tangazo la Serikali namba tatu la mwaka 1994 linaelekeza vifaa anavyopaswa kumiliki kiongozi huyo ambavyo ni bendera, orodha ya wakazi wa eneo husika na daftari la kumbukumbu.

Kimsingi, hakuna mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa hata mmoja anayeweza kukubali kunyang’anywa muhuri wake, pili hoja hii si mpya kwa sababu iliwahi kuibuka mwaka 1994 lakini ikafa kifo cha mende.

Kwa sababu mihuri ndiyo inawapa hadhi wenyeviti, kwa hiyo kitendo cha Serikali kutaka kuwanyang’anya ni kama vile walitaka kuwageuza kuwa nyoka wa kibisa.

Kwa maana wanakuwa ni kama vile nyoka wa maonyesho ya ngoma za mazingaombwe, hawana sumu kiasi kwamba hata watoto wadogo wanaweza kuwachezea na hawawezi kuwang’ata.

Kwamba wanawaondolea ile hadhi, nguvu au mamlaka ya kuwatumikia wananchi waliowachagua katika mitaa yao.

Kwamba Serikali ilikuwa inawadhalilisha kwa kuwang’oa meno na kuwafanya wawe vibogoyo. Lakini wenyeviti hao wakashtuka na wakagoma licha ya kwamba suala la mihuri haliko katika kifungu chochote cha Katiba ya nchi kinachosema ni lazima wawe nayo.

Hata hivyo, wenyeviti hao wanajenga hoja ya uhaba wa maofisa watendaji kwa sababu katika baadhi ya maeneo unakuta mtendaji mmoja anaisimamia mitaa mitatu.

Pia watendaji wengi hawakai ofisini kwao katika mitaa kwa muda mrefu kutokana na semina na utoro, sasa ni lazima wenyeviti wawe na mihuri ili kuwatumikia wananchi.

Mbali na hayo, kuna jambo moja la kujiuliza hapa kwamba wenyeviti hao walitaka kunyang’anywa mihuri kwa kuwa haujatamkwa katika sheria, je, kwanini hawanyang’anywi viti na meza na ofisi kwa kuwa navyo havijatamkwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles