Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
WAKATI msako wa watumishi hewa ukiwa umeshika kasi nchini, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), limewataka watu wote wanaojijua wazi kuwa wanamiliki vyeti bandia kujisalimisha wenyewe.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Charles Msonde, alitoa tangazo hilo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo pia alitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha sita na ya ualimu.
“Necta ndiyo yenye dhamana ya kutoa vyeti vyote vya watahiniwa wanaomaliza mitihani ya Taifa nchini, kulikuwa na changamoto ya vyeti feki (bandia) kwa kipindi kirefu. Ilipofika mwaka 2008 tulibadili utaratibu wa utoaji wa vyeti hivyo.
“Tangu wakati huo utaratibu ni kwamba lazima vyeti hivyo viwekwe picha ya mtahiniwa na kwa jinsi mfumo wetu ulivyo mtu yeyote ambaye anamiliki cheti feki lazima tutambaini popote alipo.
“Hivyo nichukue fursa hii kuwajulisha wale wanaojijua kuwa wanamiliki vyeti feki na wanavitumia kuombea nafasi mbalimbali za kazi wajitokeze na kujisalimisha maana tutamkamata tu na sheria itachukua mkondo wake,” alisema.