Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Shirikisho la Wenye Viwanda Tanzania (CTI) wametaka mikakati ya ziada kukabiliana na pombe haramu ili kulinda sekta hiyo nchini.
Wenye viwanda hao wamebainisha hayo leo Februari 17,2025 wakati wa mkutano wa wadau uliokuwa ukijadili athari na changamoto kutokana na utengenezaji, matumizi na usambazaji wa pombe haramu.
Akizungumza katika mahoajiano na waandishi wa habari Mwenyekiti Mstaafu wa CTI, Paul Makanza, amesema wanashirikiana na wadau wote kama vile Tume ya Ushindani (FCC), Shirika la Viwango (TBS) ili kuhakikisha tatizo la pombe haramu linapata ufumbuzi.
“Pombe haramu ni tatizo kubwa dunia nzima, inaathiri afya za watumiaji kwa sababu hazijapitia kwenye ‘process’ kama zingine zinavyotengenezwa, zinaathiri viwanda ambavyo vinalipa kodi, vinatoa ajira na vinatunza mazingira,” amesema Makanza.
Naye Mkurugenzi wa Uhusiano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), John Wanyancha, amesema wazalishaji wanapoteza fursa ya kuuza bidhaa halali kutokana na kuwepo kwa pombe haramu sokoni.
Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora kutoka Shirika la Viwango nchini (TBS), Lazaro Msasalaga, amesema kupitia Kurugenzi ya Udhibiti Ubora Kitengo cha Uchambuzi Vihatarishi wanadhibiti bidhaa za pombe na kusisitiza kuwa hakuna anayeruhusiwa kuuza bidhaa ambayo haijathibitishwa ubora wake.
“Tunao utaratibu wa kuhakikisha viwanda vinapoanzishwa tunapata taarifa na kwenda kuvikagua na kupima sampuli kwenye maabara, tukijiridhisha viko sawa tunatoa leseni kumruhusu mzalishaji aweze kutumia nembo yetu ya ubora kwenye bidhaa yake,” amesema Msasalaga.
Shirikisho hilo limependekeza kuimarisha utekelezaji wa sheria dhidi ya uzalishaji na usambazaji wa pombe haramu, kuongeza uelewa wa umma kuhusu madhara ya pombe zisizodhibitiwa, kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali ili kuweka mazingira bora ya biashara na kuhamasisha unywaji wa pombe kwa uwajibikaji na kuwalinda wananchi dhidi ya bidhaa hatari.