26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Wenye mashamba, viongozi wapigwa Stop kuzuia uchimbaji madini

Na Derick Milton, Simiyu

Wamiliki wa mashamba katika migodi ya dhahabu ya Bulumbaka na Lubaga katika Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, wametakiwa kuacha mara moja vitendo vya kuzuia shughuli za uchimbaji katika migodi hiyo.

Mbali na wamiliki hao, wengine ni viongozi wa vijiji na vitongoji ambako migodi hiyo ipo, ambao nao wametakiwa kutojihusisha na vitendo hivyo ambavyo vimekidhiri kwenye migodi hiyo na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.

Onyo hilo limetolewa Februari 19, na Afisa Madini Mkoani huo, Mhandisi Joseph Kumbulu, wakati akizungumza na wachimbaji wadodo wa migodi hiyo wakiwemo wamiliki wadogo, wanunuzi wadogo wa dhahabu katika mkutano uliofanyika katika Kijiji cha Dutwa Wilayani humo.

Mhandisi Kumbulu amesema kuwa vitendo hivyo vimekithiri na kuwa kero, ambapo wamiliki wa mashamba kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji wamekuwa wakizuia uchimbaji kwa watu waliopewa leseni na tume ya Madini.

Amesema kuwa vitendo hivyo ambavyo vinafanywa na watu hao ni kinyume cha Sheria, kwani wao hawana Mamlaka yoyote ya kufanya hivyo na wala wao siyo wamiliki wa Madini kwa mujibu wa Sheria.

“Mtu au kikundi chochote kikiomba leseni hakuna Sheria ambayo inasema lazima aanzie kwa watu wenye mashamba au viongozi wa vijiji, mtu akiomba leseni tume ya Madini na akapewa anatakiwa kabla ya kuanza uchimbaji akafanye mazungumzo kwanza na mwenye shamba ili wakubaliane jinsi gani wote watanufaika.

“Lakini kumzuia asichimbe hilo ni kosa kubwa, Madini ni mali ya serikali, mwenye shamba yeye anamiliki ardhi tu ya juu lakini Madini siyo ya kwake, hivyo leseni ikitoka lazima mwenye hiyo leseni na ni sharti, afanye mazungumzo kwanza na mwenye shamba,” amesema Mhandisi Kumbulu.

Ofisa Madini huyo amesema kuwa migogoro baina ya wenye mashamba, viongozi wa vijij na wenye leseni imekuwa ya mara kwa mara kwenye migodi hiyo huku chanzo kikubwa ikiwa wengi wao kutokuwa na elimu juu ya Sheria za Madini.

“Kama ofisi tumetoa elimu kwa makundi yote wakiwemo wamiliki wa mashamba, kuanzia sasa ni marufuku kuzuia uchimbaji, mtu yeyote ambaye atahusika hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, sasa hivi hatutaongea bali ni mtu kumchukulia hatua,” ameongeza Mhandisi Kumbulu..

Aidha, ametaka watu wanaopewa leseni za kuendesha migodi hiyo kuhakikisha wanatimiza masharti ya kufanya mazungumzo na wenye mashamba, kama utaratibu ulivyo ili kumaliza Migogoro ya mara kwa mara.

Katika hatua nyingine Mhandisi Kumbulu amesema kuwa ofisi yake imewazuia wanunuzi wadogo wa dhahabu zaidi ya 100 kufanya shughuli hiyo katika mkoa huo kutokana na kutokuwa na namba ya mlipakodi (TIN Number).

Kumbulu amesema kuwa wamebaini uwepo wa wanunuzi wengi wadogo wa Madini ambao wamekuwa wakifanya biashara hiyo bila ya namba ya mlipakodi, kutokuwa na risiti pamoja na kutokuwa na daftari la mahesabu hali ambayo imefanya kuzuia leseni zao mpaka pale watakapokamilisha vitu hivyo.

Awali akiongea katika kikao hicho Mwenyekiti wa Chama cha wachimbaji wadogo katika mkoa huo Paul Zabron, aliwataka wachimbaji hao kuacha kupelekea malalamiko yao kwa viongozi wa serikali na badala yake wayawasilishw kwenye Chama chao na kutatuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles