PATRICIA KIMELEMETA NA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM
WAFANYABIASHARA wakubwa wenye maduka mitaa ya Kariakoo na Karume wamewapa wamachinga bidhaa zao waweze kuziuza nje ya maduka yao, MTANZANIA limebaini.
Hali hiyo imetokea ikiwa ni siku ya pili baada ya Rais Dk John Magufuli kutoa agizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya kutowafukuza wamachinga katikati ya miji bila kuwapatia maeneo rafiki ya biashara.
Uchunguzi uliofanywa na MTANZANIA jijini Dar es Salaam, umebaini kuwapo shehena kubwa za bidhaa mbalimbali zinazouzwa na wamachinga kwa makubaliano maalum na wenye maduka.
Bidhaa hizo ni pamoja na nguo za aina mbalimbali, viatu, mikoba ya wanawake, vipodozi, nywele bandia, vyombo vya nyumbani na vifaa vya umeme na ujenzi.
Vingine ni vyakula na matunda ya kila aina ambayo yamemwagwa katika mitaa mbalimbali ya Kariakoo kusubiri wateja.
Uchunguzi huo umebaini kuwa bidhaa hizo zinauzwa kwa bei nafuu tofauti na madukani au kwenye masoko yaliyo rasmi.
Mathalani nguo zilizokuwa zikiuzwa kati ya Sh 30,000 hadi Sh 50,000 dukani hivi sasa zinauzwa kwa wastani wa Sh 10,000 hadi Sh 20,000.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya uchumi wameieleza hali hiyo kuwa inaweza kuporomosha uchumi kwa kuwa bidhaa hizo wanazopewa wamachinga kwa kile kinachoitwa ‘mali kauli’, hazitalipiwa kodi kama ilivyotarajiwa.
VYOO CHANGAMOTO
Wakati huohuo, uhaba wa vyoo katika mitaa ya inayozunguka eneo la Kariakoo ikiwamo Kongo, Nyamwezi, Tandamti, Swahili, Sikukuu, Narung’ombe Mchikichi na unaweza kuibua tatizo jipya la afya.
Katika mitaa hiyo hakuna vyoo rasmi vinavyoweza kuhimili na kutosheleza wingi wa wafanyabiashara hao na wateja wao.
Katika uchunguzi huo imebainika kuwa majengo mengi ya biashara yaliyopo Kariakoo yana vyoo vichache kwa ajili ya wapangaji wao na mengine hayana.
Kutokana na hali hiyo baadhi ya wafanyabiashara wanaamua kujisaidia haja ndogo kwenye chupa za plastiki na kuzitupa ovyo mitaani.
Katika Soko Kuu la Kariakoo miundombinu ya vyoo vyake ni ya zamani hivyo haikidhi mahitaji ya wateja wake.
HALMASHAURI YA ILALA
Akizungumzia hali hiyo, mmoja wa maofisa wa halmashauri ya Ilala ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa sababu maalum, alisema vyoo vya umma katika halmashauri hiyo vimefungwa kwa sababu ya ubovu wa miundombinu yake ambayo ni ya zamani tofauti na mahitaji ya sasa.
“Miundombinu ya vyoo vyetu vya umma katika masoko ya Kariakoo, Karume imepitwa na wakati.
“Vimefungwa na havifai kwa matumizi ya binadamu ingawa awali vyoo hivyo vilikuwa vikichangia mapato ya ndani,“ alisema ofisa huyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Dar es Salaam jana, baadhi ya wasomi ambao walionyesha wasiwasi wao kuhusu wafanyabiashara hao kufurika katikati ya miji.
Mkurugenzi wa Taasisi ya utafiti wa uchumi na kuondoa umaskini nchini (REPOA), Profesa Samuel Wangwe alisema mpaka sasa huduma za vyoo na msongamano wa watu katika mitaa ya Kariakoo ni mbaya kuliko ilivyokuwa awali, jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
“Idadi ya vibaka na wezi imeongezeka kutokana na msongamano mkubwa wa watu kwenye maeneo hayo.
“Kunaweza kutokea magonjwa ya mlipuko hivyo mamlaka husika zinapaswa kukaa na kuangalia hali hiyo,”alisema Profesa Wangwe.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Profesa Hajji Semboja alisema kauli ya Rais Magufuli kuhusu wamachinga imetafsiriwa vibaya na watendaji wake.
Alisema rais alimaanisha mamlaka husika kutenga maeneo maalumu ambayo yatakuwa na huduma zote zinazostahili kwa ajili ya kufanyia shughuli zao.
Alisema kitendo cha wamachinga kurudi kwenye maeneo yasiyo rasmi hadi barabarani kinaonyesha wazi kuwa bado kuna tatizo la uelewa kwa wafanyabiashara hao.
Katika maeneo hayo, lazima kuwe na utaratibu maalumu ambao utasaidia serikali kukusanya kodi kwa wafanyabiashara hao, alisema.
Hata hivyo, Dk. Honest Ngowi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, alisema wamachinga wanapaswa kutengewa maeneo maalumu ya kufanya shughuli zao kurahisisha ukusanyaji wa kodi.