KOCHA wa Arsenal, Arsene Wenger, amedai kwamba hana wasiwasi na maneno ya mashabiki ya kumtaka aondoke katika klabu hiyo.
Kutokana na matokeo ambayo klabu hiyo iliyapata katika mchezo wake mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Tottenham ya 2-2, baadhi ya mashabiki walimtumia ujumbe kocha huyo kwamba anatakiwa kuondoka hasa akishindwa kuchukua ubingwa msimu huu.
Tangu Februari mwaka huu, Arsenal ilipoifunga Leicester City mabao 2-1, imecheza michezo mitano bila ya kupata ushindi katika michuano mbalimbali.
“Angalia nimekuwa hapa kwa miaka 19 sasa, nimekaa miaka yote hiyo kutokana na ubora wangu huku nikiwa kocha sahihi wa timu hii.
“Nimezoea maneno ya watu kwa kipindi chote hicho na bado naweza kuendelea kuwa katika ubora wangu hadi miaka 35 ijayo.
“Kutokana na hali hiyo sina wasiwasi na wanahabari wanachokisema na mashabiki kwa kuwa ni hali ya kawaida katika maisha ya soka, lakini mwisho wa msimu kila kitu kitaeleweka,” alisema Wenger.