MSHAMBULIAJI wa klabu ya Arsenal, Danny Welbeck, atakuwa nje ya uwanja kwa miezi mitatu hadi mitano kutokana na kusumbuliwa na goti.
Mchezaji huyo wa timu ya Taifa ya England pia ataikosa michuano ya Euro ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi majira ya joto nchini Ufaransa na atashindwa kuungana na klabu yake katika maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu ambapo Arsenal inatarajia kwenda Marekani.
Welbeck alipata maumivu ya goti katika mchezo wa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati klabu yake ikipambana na Manchester City alipogongana na Bacary Sagna, mchezo huo ulimalizika kwa sare ya 2-2.
Hata hivyo, kocha wa England, Roy Hodgson, amesema kwamba kumkosa mchezaji huyo katika kikosi chake kutakuwa na pengo kubwa.
“Welbeck ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa katika safu ya ushambuliaji, kumkosa kwake ni tatizo kwetu katika michuano ya Euro, lakini bado tuna kikosi kipana ambacho kitaweza kupambana na kufanya vizuri,” alisema Hodgson.