WEKENI AKIBA YA MAHINDI KUEPUKA NJAA-RC

0
803

Na TIGANYA VINCENT

-TABORA

WAKAZI wa Mkoa wa Tabora wametakiwa kuwa na akiba ya kutosha ya chakula kabla hawajafanya maamuzi ya kuuza mahindi yao, ili kuepuka kukumbwa na njaa.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri, wakati wa mkutano na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo walipokuwa wakitathmini hali ya chakula.

Kufuatia kuwapo kwa upungufu wa chakula, Mkuu wa Mkoa ametoa fomu maalumu kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi Watendaji ili mtu anayetaka kuuza chakula ajaze kabla ya kuuza kuelezea hali halisi ya chakula katika familia yake na iwapo kinachobaki kitamfikisha msimu wa mavuno mengine.

Alisema kuwa, lengo ni kutaka kudhibiti watu wanaouza ovyo chakula na wanapopungukiwa chakula na kukabiliwa njaa wanatupa lawana kwa Serikali kwamba haitaki kuwasaidia.

Mkuu huyo wa Mkoa alisema kuwa, fomu hizo zinataka anayeuza chakula ni yule tu mwenye ziada na si vinginevyo.

Aliongeza kuwa, ili kuepuka udanganyifu, fomu hizo ni lazima zijazwe na muuzaji, mnunuzi, Mtendaji wa Kijiji, Mtendaji wa Kata na kisha nakala zipelekwe katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Wilaya na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ili kama ikitokea mtu anahitaji msaada wa chakula awe ni yule ambaye hakuuza chakula.

Mwanri alisisitiza kuwa, Serikali ya Mkoa haimzuii mtu kuuza mahindi yake, lakini lazima anayefanya hivyo awe ni yule mwenye ziada.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Dk. Thea Ntara, alisema mahitaji ya Mkoa huo toka mavuno hadi mavuno ni tani 605,864 za nafaka aina ya mahindi, lakini mavuno ya mwaka huu ni tani 445,362, ikiwa ni pungufu ya tani 160,502 za mahindi.

Alisema kufuatia hali hiyo, wananchi wanatakiwa kabla ya kuuza chakula chao ni vema wakajihakikishia kuwa na ziada ya kutosha kwa ajili ya matumizi ya familia zao kwa kipindi chote hadi mavuno mengine.

Dk. Ntara alitoa wito kwa wakazi wa Tabora ambao hawakupata mavuno mazuri kutumia muda huu kununua kwa wingi chakula kwa ajili ya kujiwekea akiba,  kwa kuwa bei bado iko chini.

Mkoa wa Tabora ulipata mvua kwa kipindi cha miezi miwili tu, kitu kilichosababisha baadhi ya mazao kushindwa kukomaa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here