Waziri Zanzibar ataka ushirikiano Sekta ya Utalii

0
581

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale, Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo ameomba kuwapo kwa ushirikiano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara katika sekta ya utalii.

Amesema hayo leo jijini Dar es Salaam, katika Onyesho la Kiswahili la Utalii la Kimataifa ambapo pamoja na mambo mengine ametaka sekta hiyo ipewe kipaumbele kama sekta nyingine kwa upande wa Zanzibar.

“Lazima tufanye kazi kama watoto pacha, kwa sababu watalii 100 mnaopata huku 28 wanakuja Zanzibar katika siku zile za mwisho.

“Utafiti umefanywa na kampuni mbalimbali za utafiti na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa hiyo watalii wakija huku na sisi ile bakaa inatudondokea tunapata riziki yetu,” amesema Kombo.

Amesema kwa upande wa Zanzibar sekta ya utalii tayari Rais Dk. Mohamed Shein ameipa kipaumbele na asilimia 30 ya pato la taifa na mchango wa uchumi wa Zanzibar kwa mtu mmoja mmoja inachangiwa na utalii hata zao la karafuu limepitwa tayari huku watalii 500,000 wakitembelea na kuwafanya kuvuka lengo na mwaka huu wameendelea hadi kufikia 700,000.

“Lakini watalii wa moja kwa moja wa kigeni ni asilimia 80 na zaidi, na kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana utalii umechangia moja kwa moja Dola milioni 476 ambayo ni kubwa inakaribia hata bajeti yetu, kwa hiyo kule utalii umeshapewa kipaumbele kikubwa sana.

“Huku najua mna sekta nyingi, mna madini, viwanda lakini kule sisi sekta zilizopo kidogo ni chache, sasa hivi ndiyo kidogo mambo mengine yale yameanza lakini huku mnajitahidi sana,” amesema Kombo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here