Waziri wa Ulinzi wa Sudan Awadh Ibn Auf ameapishwa kuwa rais wa baraza la mpito la kijeshi ambalo kulingana na jeshi litaongoza kwa kipindi cha miaka miwili ya mpito.
Kituo cha radio kinachomilikiwa na serikali kimearifu kuwa mkuu wa majeshi Kamal Andel-Marouf ameapishwa kuwa makamu wa rais wa baraza hilo.
Hatua hii imekuja huku waandamanaji wakilalamika kwamba utawala huo wa kijeshi haukumaanisha mabadiliko, na kuahidi kuendelea kuandamana hata baada ya hapo jana kutangazwa kwa sheria inayozuia raia kutembea usiku wa kuanzia saa 4 hadi saa 10 alfajiri.
Rais Omar al Bashir wa Sudan aliyetawala kwa miaka 30, jana Alhamisi alipinduliwa na kukamatwa kufuatia miezi kadhaa ya maandamano ya kuipinga serikali. Rais Omar al-Bashir aliyetawala Sudan kwa miaka 30 amepinduliwa na kukamatwa baada ya miezi kadhaa ya maandamano makubwa yaliyoipinga serikali.
Kwa upande mwingine, makundi ya upinzani nchini humo yametoa wito kwa waandamanaji kusalia mitaani wakipinga mapinduzi hayo ya kijeshi. Kundi hilo lililozungumza kwa niaba ya waratibu wa maandamano hayo wamesema kwenye taarifa yao kwamba mapinduzi pamoja na kusimikwa kwa utawala wa kijeshi wa mpito kwa namna yoyote hakukuashiria mabadiliko.
Waandamanaji waliendelea kukaa mbele ya makao makuu ya jeshi ikiwa ni siku ya sita mfululizo, wakati sheria iliyotangazwa na jeshi ya kutotembea nje kuanzia majira ya saa 4 za usiku ikiwa imeanza kutekelezwa nchini humo, licha ya kuongezeka kwa mbinyo wa jamii ya kimataifa dhidi ya jeshi wakitaka wakabidhi madaraka kwa raia. Awali jeshi liliwaonya raia kutopuuza tangazo hilo.
Umoja wa Ulaya ameliomba jeshi la Sudan kufanya mabadilishano hayo ya madaraka haraka. Mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya, Federica Mogherini amesema mchakato wa siasa wa kuaminika na jumuishi ndio pekee utakaofanikisha kufikiwa kwa matarajio ya watu wa Sudan.
Msemaji wa katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, Guterres ametoa mwito wa mabadilishano yatakayokidhi matarajio ya kidemokrasia miongoni mwa watu wa Sudan.