WAZIRI WA UGANDA AKUNWA NA MWENDOKASI DAR

0
517
Bagiire Henry
Bagiire Henry

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

WAZIRI anayeshughulikia masuala ya usafirishaji nchini Uganda, Bagiire Henry, ameusifu mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) kwa kurahisisha huduma ya usafiri kwa wananchi waliopo katika Jiji la Dar es Salaam na kuahidi kuutekeleza nchini kwao.

Akizungumza mara baada ya kutembelea mradi huo kutoka eneo la Kivukoni hadi kituo cha Morocco, Bagiire, ambaye aliongoza ujumbe wa Serikali ya Uganda kuja nchini, alisema mradi wa BRT umekuwa na mafanikio makubwa katika Jiji la Dar es Salaam, kwani umesaidia kuondoa msongamano mkubwa wa magari.

Alisema hata Uganda wana mpango wa kuanzisha mfumo huo, ili uweze kukabiliana na ongezeko kubwa la watu linalokua kwa kasi katika Jiji la Kampala.

“Tumefurahi kuuona mfumo wenu wa mabasi yaendayo haraka unavyofanya kazi, nasi tukirudi Uganda tutakwenda kutekeleza kile tulichokiona,” alisema Bagiire.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuriho, ambaye alimwakilisha Waziri Profesa Makame Mbarawa, alisema mradi wa BRT umekuwa kivutio kikubwa cha wageni, ndiyo maana viongozi hao kutoka Uganda waliomba kuutembelea.

Dk. Chamuriho alitumia fursa hiyo kuwataka wakazi wa Dar es Salaam na watumiaji wa mabasi ya BRT kutunza miundombinu yake ili mradi huo weze kudumu na kuleta manufaa zaidi kwa Watanzania.

Naye Mkurugenzi wa Uendeshaji na Usimamizi wa Miundombinu kutoka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka, (DART), Mhandisi John Shau, amewashukuru wageni hao kutoka Uganda kwa kutembelea mradi huo.

Alisema mradi huo umekuwa wa mfano na wa kwanza kutekelezwa katika nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Hivi karibuni Jiji la Dar es Salaam kupitia BRT, lilipata tuzo ya mwaka ya usafirishaji endelevu duniani, baada ya kuondoa msongamano mkubwa wa magari na kuwawezesha wananchi kutumia muda mfupi zaidi, ikilinganishwa na hapo awali ambapo walikuwa wakitumia muda mrefu kwa kutumia usafiri wa daladala.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here