23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI WA JK APANDISHWA KORTINI DAR

Na Kulwa Mzee-Dar es Salaam


ALIYEKUWA Naibu Waziri wa Kilimo na Chakula wa Serikali ya Awamu ya Nne, Adam Malima na dereva wake wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kumzuia Polisi kufanya kazi yake.

Washtakiwa hao, Malima na Ramadhani Kwagwande walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicius Mwijage na kusomewa mashtaka na Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono.

Kombakono alidai shtaka la kwanza linamkabili Ramadhani, anayedaiwa Mei 15 mwaka huu maeneo ya Masaki kwa nia ya kukataa kukamatwa kwa kuegesha gari lenye namba T 587 DDL vibaya, alimjeruhi Ofisa wa Kampuni ya Priscane Business Enterprises, Mwita Joseph na kumsababishia maumivu ya mwili.

Shtaka la pili la shambulio linamkabili Malima ambapo anadaiwa katika tarehe hiyo na eneo hilo alimzuia askari polisi Abdul mwenye namba H 7818,  kufanya kazi yake ya kumkamata Ramadhani ambaye alifanya kosa la kujeruhi.

Washtakiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo maeneo ya  Masaki karibu na Hoteli ya Double Tree, ambapo baada ya kusomewa mashtaka, wote wakiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala walikana mashtaka, upelelezi haujakamilika na Jamhuri hawakuwa na pingamizi kwa washtakiwa kupata dhamana.

Hakimu Mwijage aliamuru kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja, mwenye barua ya utambulisho kutoka ofisi yoyote inayotambulika na wasaini dhamana ya maandishi ya Sh milioni tano.

Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana, wako nje kwa dhamana.

Wakili Kibatala aliifahamisha mahakama kwamba kesi itakapokuja kwa mara nyingine atawasilisha pingamizi kuhusu shtaka linalomkabili Malima.

Kibatala alidai shtaka linadai shambulio lakini maelezo ya shtaka yanaelezea kuhusu kuzuia Polisi kufanya kazi yake.

Alidai shtaka na maelezo vinatofautiana hivyo atawasilisha pingamizi kuomba shtaka hilo lifutwe. Kesi iliahirishwa hadi Juni 15 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, amemwagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, afuatilie tukio la askari polisi mmoja jijini Dar es Salaam, aliyemtisha kwa risasi Malima ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Fedha katika serikali hiyo ya awamu ya nne.

Akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma jana, Mwigulu alisema amelazimika kutoa agizo hilo ili ajue ukweli wa tukio hilo.

“Nimemwagiza IGP alifuatilie tukio hilo na baadaye anipe taarifa sahihi kwa sababu hadi sasa silijui kwa undani. Ile ‘clip’ ya majibizano na jinsi risasi ilivyorushwa nimeshaiona, lakini tatizo lililopo ni kwamba, sijui walianza anzaje hadi kufikia hatua ya polisi kurusha risasi hewani.

“Kwa hiyo, nawaomba mnivumilie kidogo, nisubiri taarifa kutoka kwa IGP na baadaye nitawapa taarifa sahihi,” alisema Waziri Mwigulu kwa kifupi.

Wakati Mwigulu akisema hayo, awali Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago (Chadema), aliomba mwongozo kwa Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Zungu akitaka kujua ni hatua gani zitachukuliwa na Serikali ili kukabiliana na matumizi ya silaha hadharani.

Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema kama lisingemkamata Malima ingekuwa aibu kwa jeshi hilo na askari husika wangeshtakiwa kwa woga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema Malima na dereva wake walikuwa wanawazuia polisi wasifanye kazi yao.

“Polisi walilazimika kufyatua risasi tatu hewani kutokana na mazingira yaliyokuwepo ambayo yalikuwa ni hatarishi. Ingekuwa ni aibu na tungewashtaki wao (askari) kwa kushindwa kukamata washtakiwa na kupeleka kielelezo kunakotakiwa.

“Sisi polisi kama kuna mtuhumiwa na kielelezo ni lazima utumie nguvu ya kadiri kuhakikisha anakwenda kituo cha polisi na usipofanya hivyo utashtakiwa kwa woga,” alisema Sirro.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles