23.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri: Utekelezaji programu ya urasimishaji ujuzi umeanza kujibu

Mwandishi wetu -Tanga

PROGRAMU ya ukuzaji ujuzi inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, imekuwa ni chachu ya mafanikio kwa vijana katika kukuza ujuzi wao kupitia mafunzo mbalimbali ya ufundi stadi ambayo yamewajengea uwezo wa kujiajiri au kuajiriwa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Programu ya Urasimishaji Ujuzi kwa mwaka 2019/20 jijini Tanga jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema Serikali iliandaa programu hii ya kitaifa ya miaka mitano ya kukuza ujuzi kwa nguvu kazi ambapo utekelezaji wake umeanza kutoa fursa kwa vijana kupata ujuzi katika sekta mbalimbali.

“Programu hii imewasaidia vijana kupata kazi zenye staha na imewafanya waweze kuwa washindani katika soko la ajira sambamba na kuongeza tija mahali pa kazi kwa kuwa waajiri wamekuwa wakipata wafanyakazi wenye viwango vya ujuzi unaotambulika,” alisema Mhagama.

Alisema utambuzi na urasimishaji ujuzi una lengo la kutambua, kutathmini na kurasimisha ujuzi uliopatikana kupitia nje ya mfumo rasmi wa mafunzo, hivyo kupitia programu hii taaluma na ujuzi wa vijana utatambulika na wataweza kupata ajira.

“Serikali imekuwa na mikakati ya kujenga taifa lenye viwanda vingi vitakavyokuwa vinatoa asilimia 40 ya ajira kwa vijana wasiokuwa na ajira, hivyo ili kufikia azma hiyo, nguvu kazi yenye ujuzi rasmi na unaotambulika, itakuwa na manufaa katika soko la ajira,” alisema Mhagama

Kutokana na hali hiyo, alitoa wito kwa vijana wenye ujuzi katika fani mbalimbali na hawana vyeti vinavyotambulisha ujuzi wao, wafike katika vyuo vya Veta vilivyopo karibu yao waweze kujiandikisha ili kurasimisha ujuzi wao.

Katika uzinduzi huo, Waziri Mhagama alitoa vyeti kwa vijana zaidi ya 500 waliopata mafunzo kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo ufundi wa magari, uhudumu wa hoteli, ufundi ujenzi, upishi na ufundi seremala.

Aliwahimiza vijana hao waliohitimu mafunzo kutumia fursa ya miradi ya kimkakati inayoanzishwa katika mkoa huo, pamoja na kuchangamkia zabuni za kutoa huduma na ufundi katika maeneo mbalimbali.

Pia Jenista aliwataka maofisa maendeleo ya vijana, maofisa biashara na maendeleo ya jamii kutoka kwenye halmashauri mbalimbali walizotoka vijana hao waliohitimu mafunzo kupatiwa msaada wa kitaalamu utakaowawezesha kuanzisha na kusajili vikundi na kampuni kisheria.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella, alisema kuwa amefarijika kuona vijana wa Mkoa wa Tanga watanufaika na programu hiyo ambayo itawajengea hamasa ya kupenda kurasimisha ujuzi wao.

“Katika Mkoa wa Tanga wanagenzi 1,015 watashiriki kwenye mafunzo hayo na takwimu zilizosomwa hapa zinaonyesha Mkoa wa Tanga utakuwa umevuka malengo kwa asilimia 5.2, nimefarijika sana,” alisema Shigella.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), Stella Ndimubenya, alisema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuwawezesha mafunzo stadi vijana, yatakayowafanya wakuze uchumi wao na kuwa na mchango katika kujenga Tanzania mpya ya viwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles