WAZIRI UMMY ATAKA FARAGHA KWA MAKONDA

0
1184

Na WAANDISHI WETU-DAR es Salaam     |    

WAKATI wanawake na wanaume waliotelekezwa na watoto wakiendelea kumiminika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amekosa na kusema hakuna faragha katika kulinda haki za watoto.

Pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amezitaka taasisi zisizo za Serikali kumshauri vema mkuu huyo wa mkoa namna ya kumaliza suala hilo na kufikishwa kwenye vyombo husika.

Akizungumza jana Dar es Salaam, Ummy alisema suala la kukosekana kwa faragha kwa watoto wanaodaiwa kutelekezwa na baba zao ni kasoro pekee katika utaratibu huo.

Ummy alitoa kauli hiyo katika mahojiano yaliyofanywa na Kituo cha runinga cha Clouds kupitia kipindi cha 360.

Alisema kinachofanywa na Makonda kipo ndani ya sheria, hata watendaji wanaowasikiliza wanawake wametoka katika idara yake isipokuwa kuna kasoro zilizojitokeza.

“Wizara ya Afya inaunga mkono jitihada hizo, lakini kasoro zilizojitokeza ni kwa baadhi ya wanawake waliotelekezwa kwenda na watoto na kutojali haki za kuwalinda katika hatua hizo za awali za mashtaka,” alisema.

Waziri Ummy alisema Makonda amefanya kitu kizuri na mwamko umekuwa mkubwa.

“Ila madawati yapo na ustawi wa jamii pia wapo, lakini wengi wamekuwa wazito kwenda, sasa wameitikia wito kwa kuwa yeye amewahimiza wanawake wenye matatizo hayo wafike kwake, kazi imekuwa nyepesi kwani hata wanaohudumia pale ni watu wetu wa Ustawi wa Jamii,” alisema Ummy.

Alitoa wito kwa wanawake wanaokwenda kutoa mashtaka yao kuhakikisha wanalinda haki za watoto wao kwa kutowaonyesha hadharani.

“Ninasema hili ni kosa la mwanamke mwenyewe, kwa mfano yule mtoto Mchina nimesikitika sana, kule ni kumnyanyapaa, amesambazwa mitandaoni kila mahali anazungumziwa, niwaombe Watanzania tujitahidi kuwalinda watoto hawa, tusisambaze picha zao kwa masilahi mazuri ya mtoto,” alisema Ummy. 

MAKAMU WA RAIS

Akizungumza juzi wakati wa uzinduzi wa chanjo ya saratani ya kizazi kwa wanafunzi, Makamu wa Rais, Samia, alimpongeza Makonda kwa kuchukua hatua hiyo na kwamba takwimu na taarifa zitakazopatikana zitasaidia kufanya utafiti wa kitaifa.

“Mkuu wa Mkoa nakupongeza umeanzisha changamoto hii ambayo itakuwa ni kama utafiti wa awali wa tatizo hili, takwimu utakayoikusanya pale itatupa sura ya ukubwa wa tatizo hili nchini, pengine na mikoa mingine nayo itapenda kufanya hivyo.

“Lakini baada ya kukusanya taarifa za awali, nikuombe kuwaelekeza katika njia zile rasmi za kutatua matatizo hayo na niwaombe taasisi zisizo za kiserikali wamuunge mkono Mkuu wa Mkoa kumwelekeza, kuelekeza tatizo hili katika njia rasmi.

“Kwa sababu tukikaa na kulitia dosari zoezi hili ambalo litatupa takwimu za maana za awali haitasaidia jamii, niombe sana tumsaidie baada ya kupata takwimu za awali, ielekee wapi, nini kingine kinafuata.

“Ninajua katika zoezi lile kuna maofisa ustawi wa jamii pale, baada ya kupata takwimu hizi walibebe na kulifanyia kazi katika maofisi yao na lile la kupeleka mahakamani lipelekwe, watakaokubali kumalizana baina ya wazazi wawili wamalizane, lakini kwa vyovyote vile lifanyiwe kazi liishe na kila upande uweze kuwajibika.

“Chonde sana wanaume wa Tanzania, watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, tutakapowanyima huduma wasipokuwa watoto wa maana wakawa wanaranda mitaani wanakuwa wezi, majambazi, dhima ile unaibeba wewe baba mzazi.

“Kwa sababu mama peke yake amejitahidi kutunza wale watoto, na hali ya uchumi ilivyo anashindwa kuwamudu wote, na mtoto huyu akifika miaka 16, 17, 18 si rahisi kufuata yale unayomwelekeza, wote tuwajibike hata kama mtoto huyu ulimzaa bila matakwa yako, lazima atuzwe, ahudumiwe awe mtoto mwema kwa taifa baadae,” alisema. 

BUNGE LATIKISWA

Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema kiti chake kimetikiswa na taarifa za mambo yanayoendelea Dar es Salaam, juu ya wanaume waliotelekeza watoto.

Akiahirisha kikao cha Bunge juzi usiku, Ndugai alisema amesikia baadhi ya wabunge wanaume wametajwa kwenye jambo hilo na kwamba kama wanawake hao wana uhakika na madai yao, wafike ofisini kwake na nakala ya vipimo vya vinasaba (DNA).

Huku wabunge, hasa wanawake wakiwa wanaangua kicheko, Ndugai alisema pia kama kuna wanaume ambao wametelekezewa watoto na wabunge wanawake, nao kama wana uthibitisho wa DNA wafike ofisini kwake.

“Kule Dar es Salaam kuna zoezi linaendelea, huko sasa kidogo kiti cha Spika kimetikiswa hivi. Tunatuhumiwa mahali, kidogo tumeguswa hivi, kwahiyo natarajia kupata ushauri wenu waheshimiwa tunafanyaje katika mazingira haya, kwa maana kuna watoto wetu wako barabarani.

“Haiwezekani hata kidogo, kwahiyo kina mama wale inabidi tufanye utaratibu tujue nini tutafanya, lakini pia kuna kina baba wamejitokeza huko, nimesikia na baadhi ya walalamikiwa ni kina mama wabunge, kwahiyo hili jambo halina upande.

“Hawa kina mama kama wapo, basi waje kwa Spika au wamwandikie Spika, lakini waniletee na ‘DNA test certificate’ ili tuone namna gani ya kuwezesha,” alisema Ndugai.

MAKONDA

Jana Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda, alitangaza kuwapatia bima ya afya watoto 5,000 waliofika ofisini kwake na mzazi mmoja.

Akizungumza na wanawake waliofika ofisini kwake kupata usaidizi wa kisheria, alisema bima hiyo itakuwa ya mtoto aliye chini ya umri wa miaka 17 na itagharimu Sh 50,400 kwa kila mtoto.

“Kuanzia kesho watoto wote waliokuja hapa wakiwa wametelekezwa watapatiwa bima za afya kila mmoja,” alisema Makonda.

Alisema hadi juzi jioni idadi ya watu 1,030 walihudumiwa, huku idadi ya watu mashuhuri waliotajwa imefika 107.

Makonda alisema hata hivyo kuna baadhi ya watu wameanza kuelewana baada ya kuona hali hiyo. 

Habari hii imeandaliwa na VERONICA ROMWALD, TUNU NASSOR NA JOHANES RESPICHIUS

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here