WAZIRI Mkuu wa Uholanzi, Mark Rutte, ameimarishiwa ulinzi kutokana na tishio la kushambuliwa au kutekwa na moja ya magenge ya wahalifu nchini humo.
Taarifa ya kiongozi huyo kuongezewa ulinzi imeripotiwa na gazeti la De Telegraaf la Uholanzi likidai kuwa tishio hilo limefanywa na kundi linalojihusisha na biashara za dawa za kulevya.
Hata hivyo, licha ya kuripotiwa hivyo, bado mamlaka za Uholanzi hazijathibitisha taarifa za Waziri Mkuu huyo kuimarishiwa ulinzi.
Tishio dhidi ya Rutte linatanguliwa na tukio la kuuawa kwa mwandishi wa habari aliyejizolea umaarufu mkubwa kwa kufichua wahalifu, Peter R de Vries.
Uholanzi imekuwa haisifiki kwa uhalifu wa kutupiana risasi lakini uhalifu unaotekelezwa na makundi umeendelea kushika kasi katika miaka ya hivi karibuni.