Na Mwandishi Maalumu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu Hassan, amewataka watumishi waliostaafu kuendelea na moyo wa kudumisha Muungano wa Tanganyika
na Zanzibar kwa vitendo.
Amesema ili kuweza kufikia kuenzi muungano huo na waasisi wake, ni muhimu kuzingatia kanuni bora za uhifadhi wa mazingira.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam jana, alipokuwa akizungumza katika hafla ya kuwaaga wastaafu wapatao 12 wa kada ya maofisa katika ofisi hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa.
Samia, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, alisema wastaafu hao wanapaswa kuendelea na moyo huo, kwani jukumu la kuudumisha Muungano na uhifadhi wa mazingira ni la kila mmoja katika jamii.
“Natambua kwamba ninyi nyote mliostaafu na mtakaostaafu ni mabalozi wazuri katika kuelimisha jamii kuhusu majukumu ya Ofisi ya Makamu wa Rais yanayohusu kuudumisha Muungano wetu pamoja na kuhifadhi mazingira,” alisema Waziri Samia na kuongeza:
“Natarajia mtakuwa mfano katika kuendeleza jitihada za kudhibiti uharibifu wa mazingira katika jamii inayowazunguka,” alisema Samia.
poa tu taifa kwanza