23.7 C
Dar es Salaam
Saturday, September 23, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri Nyongo:Nataka uchunguzi kifo cha mzee wa miaka 85

SAMWEL MWANGA,MASWA

NAIBU Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini chanzo kilichosababisha kifo  cha mkazi wa Kijiji cha Buhungukila, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Isululu Gabote (85), anayedaiwa kufa mikononi mwa polisi.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Waziri Nyongo alisema  ni vema uchunguzi ukafanywa ili kujua kilichosababisha kifo hicho kutokana na utata uliojitokeza hadi kufikia ndugu wa marehemu kukataa kuuchukua mwili kwa ajili ya mazishi.

Nyongo ambaye ni Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM) alisema tangu kifo hicho kitokee Mei 18, mwaka huu kimezua sintofahamu kati ya wananchi wa kijiji hicho na Jeshi la Polisi, huku wakiwatupia lawama

maofisa watendaji wa kata ya Bugarama, Zengo Kingi na Mtendaji wa Kijiji cha Buhungukila, Saimon Kadinda, wakiwatuhumu kuwa ndiyo chanzo cha kifo hicho.

Alisema  tukio hilo, limekuwa na utata mkubwa kutokana na Jeshi la Polisi kukana kuhusika na kifo hicho, huku ndugu wa marehemu wakidai

Mzee huyo kabla ya kufikwa na mauti alipigwa na polisi waliovamia kijiji hicho kuwasaka wananchi ambao hawajalipa mchango wa maendeleo wa wa Sh 10,000 kila mmoja.

“Kumekuwa na maneno mengi yaliyozua sintofahamu tangu kifo hiki kitokee na sasa sisi viongozi kuanzia mkuu wa wilaya,viongozi wa  polisi, viongozi wa CCM na mimi mbunge tumekuwa tukishirikiana ili kujua ukweli wake, inafika sehemu tunashindwa

kuelewana hivyo ni vizuri uchunguzi wa kidaktari ufanyike ili kuondoa utata huo,”alisema.

Alisema ni vizuri ukafanyika uchunguzi huru maana wananchi walio wengi wameonyesha wasiwasi iwapo madaktari walioko ndani ya Mkoa wa Simiyu wakahusika, huenda wakaficha ukweli wa kifo hicho kwa ajili ya polisi wanaotuhumiwa kuhusika na kifo hicho.

Naye Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Seif Shekalaghe alisema tangu tukio hilo lilipotokea alilishughulikia kwa kikamilifu kwa kusaidiana na wanafamilia.

Alisema alilazimika kupeleka daktari kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bariadi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kifo hicho na taarifa aliipokea na kuwaeleza wanafamilia na kukubaliana mazishi yafanyike.

Alisema kutokana na uamuzi, uliofikiwa juu ya kuchunguza upya kilichosababisha kifo hicho, itabidi wausafirishe mwili huo wa marehemu katika hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza.

MTANZANIA ilifika Hospitali ya Wilaya ya Maswa na kushuhudia mwili wa marehemu,Gabote ukiwa unafanyiwa maandalizi ya kusafirishwa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando, jijini Mwanza

kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,699FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles