27.1 C
Dar es Salaam
Monday, September 25, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri Ndumbaro kuinadi Tanzania katika maonesho ya Dubai Expo 2020

Na Mwandishi Maalum, Dubai

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Damas Ndumbaro amesema Serikali imejipanga kutumia Maonesho ya Dubai EXPO 2020 kuinadi Tanzania kwa lengo la kuwavutia wawekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwamo katika sekta ya utalii.

Dk. Ndumbaro ameyasemaFebruari 22, 2022 baada ya kutembelea Banda la Tanzania katika Maonesho Makubwa Dunia Expo 2020

Amesema Tanzania imejipanga kutumia vyema ushiriki katika jukwaa hilo ambapo Februari 27 mwaka huu itakuwa ni Siku ya Tanzania.

“Tumejipanga kutumia Tanzania Day kuinadi Tanzania katika sekta ya Utalii kwa mafanikio makubwa ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Katika siku hiyo Diaspora, wafanyabiashara wakubwa, mabalozi kutoka nachi mbalimbali na wadau wa utalii kutoka kona mbalilmbali za dunia watashiriki katika Siku ya Tanzania kwa lengo kuwashawishi wawekezaji kuwekeza Tanzania katika fursa mbalimbali,” amesema Dk.Ndumbaro.

Aidha, Dk. Ndumbaro ameungana na Mawaziri wengine kutoka Tanzania kushiriki katika Maonesho hayo kwa ajili ya kuongeza nguvu katika ushiriki ikiwa ni jitihada za kuinadi Tanzania katika nyanja mbalimbali za uwekezaji ikiwemo sekta ya utalii

Akiwa kwenye Banda la Tanzania, amewapongeza waoneshaji wa Banda la Tanzania katika Maonesho ya EXPO 2020 Dubai kwa kazi kubwa wanayoifanya ambapo Banda hilo limeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wageni kutokana na uwepo wa maudhui ya picha na video za vivutio mbalimbali vya Utalii, madini ya thamani na vito mbalimbali ikiwepo Tanzanite.

Pia kuna picha na video zinazoonesha historia na utamaduni wa Tanzania, mazao ya kilimo, miradi ya maendeleo, fursa za uwekezaji na maeneo ya ufundishaji wa Lugha ya Kiswahili kwa wageni wanaotembelea banda hilo.

“Muonekano wa kipekee (Branding) uliopo katika Banda la Tanzania ni mkakati wa kuinadi Tanzania katika fursa za uwekezaji katika sekta za Kilimo, Utalii, madini na Viwanda na Biashara,” amesema.

”Mimi na Mawaziri wenzangu tumekuja kuongeza nguvu kuhakikisha fursa za uwekezaji zilizopo Tanzania zinajulikana dunia kote kupitia maonesho haya ambayo yanashirikisha zaidi ya nchi 192, hivyo ni fursa kwetu kama nchi kunadi utajiri wetu ili kuvutia wawekezaji,” amesema Dk. Ndumbaro.

Dk Ndumbaro aliongeza kuwa: “Kwa kazi kubwa inayofanyika hapa inaonesha jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuimarisha diplomasia ya uchumi kwa kutangaza fursa za uwekezaji katika nyanja mbalimbali imeongeza muitikio chanya kwa wageni kuja na wanapofika hapa wana vitu mbalimbali vya kuona katika banda letu ambalo lina upekee na picha zenye uhalisia,” amesema.

Katika maonesho hayo mawaziri wengine waliowasili Dubai kwa ajili ya kunadi fursa za uwekeaji zilizopo Tanzania mbali na Dk Ndumbaro ni Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe sambamba na viongozi wengine wakiwemo Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Maliasili na utalii, uwekezaji pamoja na madini.

Pia taasisi zinazoshiriki maonesho hayo ni pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Wakala wa Huduma za Misitu Tazania (TFS).

Pia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati Zanzibar (ZURA), Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Shirika la Biashara la Zanzibar (ZSTC) na maafisa wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Abu Dhabi na Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Dubai katika nchi ya Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu.

Maonesho hayo ya kimataifa yaliyoanza Oktoba Mosi mwaka 2021 yanaendelea hadi Machi 31, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,717FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles