26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Ndalichako awataka wenye Viwanda kutekeleza Sheria za Kazi 

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, amewataka wamiliki wa maeneo ya kazi nchini kutekeleza ipasavyo sheria mbali mbali za kazi ikiwemo sheria ya afya na usalama mahali pa kazi ili kuwa na uzalishaji wenye tija na kuepukana na migogoro mahali pa kazi.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (aliyesima) akizungumza kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa masuala ya usalama na afya katika maeneo ya kazi mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, viongozi wa kiwanda cha Plascon pamoja na viongozi wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Prof. Ndalichako ametoa agizo hilo Julai 25, 2022 alipofanya ziara katika maeneo ya kazi jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na viongozi na maafisa wa Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri zinazosimamia sheria mbali mbali za kazi. 

Akiongea baada ya kufanya ziara katika viwanda vitatu vinavyojishuhulisha na utengenezaji wa rangi na mabomba, Prof. Ndalichako amebainisha kuwa wamiliki hao wanajitahidi kutekeleza matakwa ya sheria na maelekezo ya serikali lakini yapo mapungufu ambayo wanapaswa kuyarekebisha.

“Kuna baadhi ya wafanyakazi hawana vifaa kinga na wengine wanapewa lakini hawavitumii hivyo inabidi wasimamiwe na kuna baadhi ya viwanda tulivyotembelea tumebaini uwepo kiwango cha juu cha kelele ambazo zinaweza kuathiri wafanyakazi endapo hatua madhubuti za kuwakinga hazitachukuliwa,” ameeleza Prof. Ndalichako na kuongeza:

“Hivyo, nawaagiza OSHA kuja katika viwanda hivi kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa kina na kushauri jinsi ya kuboresha mifumo ya kuwalinda wafanyakazi dhidi ya vihatarishi mbali mbali vya usalama na afya,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, akipokea maelezo kutoka kwa kiongozi wa kiwanda mojawapo alichotembelea akiambatana na viongozi mbambali wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa Sheria mbalimbali za msuala ya kazi katika viwanda hivyo.

Kwa upande wa masuala ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Prof.Ndalichako amefafanua kuwa ofisi yake inapata malalamiko ya wastaafu ambapo changamoto zao zinatokana na waajiri wao wa zamani kutotimiza wajibu wao wa kuwasilisha michango kwenye mifuko husika.

“Serikali tumeamua kufuatilia kwa karibu juu ya michango ya wafanyakazi tunahitaji wazee wapate mafao yao bila usumbufu, tayari kwenye baadhi ya viwanda nimegundua hakuna uwiano kati ya idadi halisi ya wafanyakazi na kiwango cha michango kinacholipwa,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (kushoto), akifanya ukaguzi wa mifumo ya Usalama na Afya akiwa ameambatana na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda (katikati) pamoja na viongozi mbalimbali wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakati wa ziara yake iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa Sheria mbalimbali za msuala ya kazi katika maeneo ya kazi jijini Dar es Salaam.

Aidha, amewahakikishia wamiliki wa maeneo ya kazi kuwa Serikali ya awamu ya sita itaendelea kujenga mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji na kuwataka baadhi ya waajiri wanaotumia mawakala katika kuajiri wafanyakazi kuhakikisha mawakala hao wanatoa huduma hiyo kwa mujibu wa sheria na taratibu za leseni zao ikiwemo kutoa huduma ya kuajiri tu na sio kuendelea kuwasimamia wafanyakazi ikiwemo kuwalipa mishahara kwa niaba ya mwajiri.

Kwa upande wao wawakilishi wa menejimenti za maeneo ya kazi yaliyotembelewa wameishukuru serikali kwa kuendelea kujenga mazingira rafiki ya uwekezaji na biashara kupitia sera na miongozo inayotolewa na viongozi wake hususan Ofisi ya Waziri Mkuu. 

“Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kutuwekea mazingira wezeshi ambayo yamekuwa yakitufanya kuingia katika ushindani wa kibiashara lakini pia tunazishukuru Taasisi mbali mbali za serikali ikiwemo OSHA ambao wamekuwa karibu sana nasi kupitia kaguzi ambazo wamekuwa wakitufanyia na kutuelekeza namna ya kuendelea kuboresha mazingira yetu ya kazi.

“Aidha, wameanzisha mfumo wa kieletroniki ambao umetusaidia kuomba huduma mbali mbali ikiwemo leseni ya OSHA na hivyo kuokoa muda ambao ungetumika kufuata huduma hizo katika ofisi za OSHA,” amesema Elida Macha, Meneja Afya, Usalama na Mazingira wa Kampuni ya Kansai Plascon. Katika ziara hiyo, Prof.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, na viongozi mbalimbali wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu wakiwa katika kikao kifupi na viongozi wa kiwanda cha kuzalisha mabomba cha Plasco wakati wa ziara iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa Sheria mbalimbali za msuala ya kazi katika viwanda hivyo.

Ndalichako ameambatana na Kamishina wa Kazi, Suzan Mkangwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtendaji Mkuu Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dk. John Mduma pamoja na Mameneja wa NSSF kutoka Dar es salaam na Watendaji waandamizi wa ofisi yake.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, wakimsikiliza mfanyakazi wa kiwanda cha Kansai Plascon wakati wa ziara ya Waziri huyo katika maeneo mbali mbali ya kazi jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako (katikati) akiwa na viongozi wa kiwanda cha kuzalisha mabomba cha Plasco wakati wa ziara yake iliyolenga kuangalia utekelezaji wa sheria mbalimbali za masuala ya kazi.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles