31.3 C
Dar es Salaam
Thursday, November 28, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Ndaki amtaka Mkandarasi wa mradi wa maji kumaliza kazi kwa wakati

Na Samwel Mwanga, Maswa

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amemtaka Mkandarasi wa Kampuni ya Afrihost Investiment Limited anayejenga tenki la kuhifadhi maji katika mradi wa maji wa Malekano-Kadoto katika kijiji cha Mwang’handa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu kukamilisha ujenzi wa tenki hilo ifikapo Septemba 7, mwaka huu na si vinginevyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi katika wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu akitoa maelekezo kwa mafundi ujenzi(hawapo pichani)wanaojenga tenki la maji katika kijiji cha Mwang’handa kwa kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa tenki hilo.(Picha Na Samwel Mwanga).

Waziri Ndaki ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi katika Wilaya ya Maswa amesema hayo leo Jumanne Julai 26, katika kijiji cha Mwang’handa linapojengwa tenki hilo wakati alipokagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo hilo.

Amesema mara kadhaa amekuwa akipita katika eneo la ujenzi wa tenki hilo lakini amebaini ya kuwa umekuwa ukisuasua jambo ambalo linawachelewesha wananchi kupata huduma ya maji katika vijiji vitatu ambavyo ni vya Malekano, Kadoto na Mwang’handa.

Waziri Ndaki amesema chanzo cha maji kipo lakini Mkandarasi ndiye amekuwa akichelewesha ujenzi wa tenki hilo kwani lisipokamilika wananchi hawatapata huduma ya maji.

“Chanzo cha Maji kipo cha kutosha tena kwa taarifa za wataalam wa maji yapo ya kutosha lakini anayetuchelewesha ni huyu mkandarasi ambaye kazi zake ni za kusuasua.

“Mwambieni huyo Mkandarasi ambaye hayupo hapa na ametukimbia kuwa ifikapo Septemba 7, mwaka huu awe amekamilisha hii kazi kwa mujibu wa mkataba wake kinyume cha hapo aondoke kwani pesa kapewa bado anafanya mchezo mchezo mimi sitakubali,”amesema Waziri Ndaki.

Amesema Serikali kupitia Rais Samia Suluhu imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kugharamia miradi ya maji lakini bado wako baadhi ya wakandarasi waliopewa kazi za kujenga miundombinu ya maji wamekuwa wakichelewesha kazi walizopewa na hivyo kuwachelewesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama.

Awali, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini(RUWASA) wilaya ya Maswa, John Jishuli akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo amesema kuwa unatekelezwa  kupitia program ya P4R II .

Amesema mradi huo ambao uko chini ya Ruwasa ukikamilika utahudumia wananchi wa vijiji hivyo na gharama ya ujenzi wake ni  Sh 716,646,886.30 ambao ulianza Machi 7, mwaka huu na kumalizika ifikapo Septemba 7 mwaka huu.

Amesema hadi sasa Mkandarasi huyo ameshalipwa kiasi cha Sh 91,353,417.00 na kazi ambazo zimepangwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa vituo 8 vya kuchotea maji,ujenzi wa tenki lenye ujazo wa mita 135 pamoja na kuchimba mtaro wa kuweka bomba mtandao wa Kilomita 11.

“Mradi huu utahudumia watu 4,000 katika vijiji vya Malekano,Kadoto na Mwang’handa na chanzo cha maji ni kisima kirefu kilichoko kwenye kijiji cha Malekano ambacho kina kina cha Mita 70 na maji mengi ya kutosha,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles