27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

WAZIRI NCHEMBA ANG’AKA POLISI KUUA RAIA

NA GUSTAPHU HAULE- PWANI

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua askari wa Wilaya ya Bagamoyo waliofanya mauaji kwa kuwapiga risasi vijana wawili wafugaji wa kabila la Kibarbeg.

Nchemba alisema askari hao lazima wachukuliwe hatua haraka iwezekanavyo.

Tukio la kuuawa kwa vijana hao, Sainga Gheambalelega (21) na Rumay Gheambalelega (23) wote wa familia moja, lilitokea Februari 28, mwaka huu wakati askari hao walipokwenda katika kijiji hicho kutaka kuwachukua ng’ombe ili wawapeleke Kituo cha Polisi Bagamoyo.

Nchemba alitoa kauli hiyo jana wilayani hapa wakati alipokwenda kuzungumza na wafugaji wa Kijiji cha Kidomole Kata ya Fukayosi, ili kutafuta suluhu.

Ziara ya Nchemba katika kijiji hicho ilikuja baada ya familia ya vijana hao kukataa kuzika miili ya ndugu zao wakitaka kwanza wamwone Waziri Nchemba ili aweze kuwasikiliza na kuwatatulia kero zao zinazosababisha wafugaji hao kuuawa mara kwa mara katika kijiji hicho.

“Serikali haiwezi kutenganisha wafugaji na wakulima kwa kuwa wote wanategemeana na zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanajishughulisha na mambo hayo hivyo kitendo kilichofanywa na askari hao hakifai kuvumiliwa.

“Wafugaji si wavamizi kama baadhi ya watu wanavyodhani, lakini ni Watanzania ambao wameamua kujikita katika ufugaji hivyo hakuna sababu ya kuwanyanyasa na kuwaonea.

“Nimesikitishwa na kitendo hiki cha hawa askari kuwaua wafugaji hivyo lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao kwa haraka maana vitendo hivi havifai kuachwa vikaendelea katika nchi yenye amani kama hii,” alisema waziri huyo.

Katika hatua nyingine, Nchemba amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo, kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini tuhuma zinazowakabili baadhi ya askari wilayani humo.

Aidha, aliwataka wananchi pamoja na wafugaji hao kuhakikisha wanawafichua watu ambao wanashirikiana na askari kufanya vitendo visivyofaa kwa wafugaji ili wapate fedha.

Katibu wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Mashariki (CCWT), Bosco George, alimweleza waziri huyo kuwa katika kijiji hicho kuna matukio mawili ya wafugaji kuuawa na askari akikumbusha tukio la Agosti mwaka jana kwamba aliuawa Gegona Molemu na Februari 28, mwaka huu waliuawa vijana wawili huku akieleza kuwa matukio hayo yanazidisha utata na kuleta hofu kwa wafugaji.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles