Na Ramadhan Hassan,Dar es Salaam
Waziri  wa Viwanda na Biashara, Geoffrey Mwambe amewasili wafanyabiashara kuwasilisha rufaa zao, Baraza la  Ushindani nchini (FCT) iwapo hawakuridhika na maamuzi yanayotolewa na baadhi ya Mamlaka nchini
Amezitaja Mamlaka hizo kuwa ni pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Maji na Nishati(EWURA, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri na Usalama wa Anga (TCAA), Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa nchi kavu LATRA, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa juu wa Petroli (PURA).
Waziri Mwambe aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Menejimenti na Wafanyakazi wa FCT alipofanya ziara katika Baraza hilo jana, ambapo alikuwa ameambatana  na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe  pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa Wizara ya Viwanda na Biashara.
Akiwa katika ziara hiyo katika baraza hilo lenye jukumu la kupokea, kusikiliza na kuamua kesi za rufaa zinazotokana na maamuzi ya Baraza la ya Ushindani (FCT) pamoja na Mamlaka za Udhibiti,amesema wananchi wasiogope kwenda kutafuta haki katika Tume hiyo.
Amesema Baraza hilo ndilo limepewa hadhi ya kimahakama ya utoaji haki kwenye masuala ya ushindani udhibiti wa soko, kumlinda mlaji na maamuzi ya kesi za rufaa yanayotolewa na baraza hilo ni ya mwisho.
Waziri Mwambe amewataka watumishi wa Baraza la Ushindani (FCT) kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa wakati wakiwahudumia wafanyabiashara wanaofika katika baraza hilo kutafuta haki katika kesi zinazohusu biashara zao na wajiendeleze kielimu ili kuendana na wakati.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Exaud Kigahe amewapongeza watumishi wa Baraza hilo kufanya kazi vizuri ambapo amewaahidi kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara itaendelea kushirikiana na Baraza hilo ambalo ni muhimu katika kuendeleza biashara nchini ili kuliwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.