25.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mwijage: SGR haitaathiri biashara ya kusafirisha mizigo

NA AZIZA MASOUD -Dar es Salaam


WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amesema reli ya kisasa ya (SGR) haiwezi kuathiri biashara ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya barabara na amewataka wamiliki wa malori kutokuwa na hofu.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana wakati akifungua mkutano wa Chama cha Wasafirisaji (TAT).

Alisema Serikali inatambua mchango mkubwa wa wasafirishaji nchini kwa kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kuingizia mapato, hasa ya kigeni.

“Tutajenga reli ya standard gauge lakini malori bado yanaendelea kuhitajika, Uingereza na Marekani yapo licha ya nchi hizo zina reli za kisasa,” alisema.

Mwijage alisema sekta ya barabara inachangamsha uchumi wa nchi na inaajiri watu wengi kupitia nyanja mbalimbali.

Alisema mwelekeo wa Serikali ni kujenga viwanda vya kati na vikubwa ili kuchochea maendeleo ya nchi.

“Serikali imepokea na itaendelea kuzifanyia kazi changamoto zilizopo katika sekta ya usafirishaji nchini,” alisema.

Awali, Rais wa TAT, Zacharia Hanspope, alisema sekta ya usafirishaji inakumbwa na changamoto mbalimbali zikiwamo vizuizi vingi visivyo vya kodi na visivyo vya lazima katika baadhi ya barabara wanazotumia.

Alitaja changamoto nyingine ni kuwapo kwa sheria na kanuni mbalimbali za vyombo vya Serikali zinazokinzana kwa kutoa maelekezo yanayotofautiana.

Alisema changamoto nyingine ni utaratibu unaotaka wasafirishaji kutembea na risiti za malipo za kieletroniki (EFDs) katika magari yaliyobeba mizigo wakati wahusika bado hawajalipa.

Pia alisema wasafirishaji hawaridhishwi na utaratibu uliowekwa wa kuadhibu wamiliki wa magari ya kusafirisha mizigo kwa makosa yaliyofanywa na madereva.

“Ni matumaini yetu kuwa Serikali itazingatia changamoto hizi kwa undani na kuangalia namna ya kuzitatua ili tuweze kufanya biashara vizuri na kwa ufanisi zaidi jambo litakalotufanya kuchangia kwa ukamilifu juhudi za Serikali za kukuza uchumi,” alisema Hanspope.

Katika mkutano huo, wajumbe walipokea taarifa za utendaji wa chama hicho kwa mwaka mzima. Pia wamefanya uchaguzi wa viongozi wa juu baada ya waliokuwapo kumaliza muda wao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles