26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

WAZIRI MWIGAJE AKUMBUKA ALIVYONUSURIKA KUTUMBULIWA

Na Amina Omari-TANGA


WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amekumbuka namna urasimu uliokuwapo katika taasisi za wizara hiyo ulivyosababisha kuweka rehani nafasi yake ya uwaziri wakati wa ziara ya Rais Dk. John Magufuli, katika kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh.

Hayo aliyasema jana mjini hapa wakati akifungua Maonyesho ya Sita ya Biashara ya Kimataifa Mkoa wa Tanga.

Mwijage alisema vitendo vya urasimu vimekuwa vikiwakwaza wawekezaji wengi nchini.

Alisema hali hiyo imesababisha kuwapo kwa manung’uniko ya utendaji wa taasisi ambazo zipo chini ya wizara, ambayo yamekuwa chanzo cha viwanda vingi kufa na wawekezaji kushindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

“Ndugu zangu, leo (jana) nafungua maonyesho haya, lakini nikiwa nina kumbukumbu ya kutaka kuondolewa kwenye nafasi hii na Mheshimiwa Rais (John Magufuli),  kwa sababu ya watendaji wachache waliokuwa wanataka kufanya ujanja ujanja kwenye maamuzi,” alisema Mwijage.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inahitaji viwanda, hivyo ni jukumu la taasisi zinazohusika na usajili pamoja na vibali, kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri yatakayoweza kuvutia wawekezaji .

Kutokana na hali hiyo, aliagiza Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Uwakala wa Usajili wa Makampuni (Brela) na  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade), kuhakikisha wanatembelea maonyesho yote ili kutoa elimu kwa wananchi na wafanyabiashara, kuhusu hatua za kuchukua kabla ya kuanzisha kiwanda au kampuni.

“Imekuwa ni jambo la kawaida halmashauri wanapotenga maeneo ya viwanja vya viwanda kuuzwa kwa bei ya juu, niwaambie tu kwa mpango huo viwanja hivyo vitashindwa kuuzika kwa haraka kwani mchakato wa kuanzisha kiwanda unahitaji uwekezaji mkubwa, huku una mzigo wa bei kubwa ya kiwanja,” alisema.

Naye Makamu wa Rais Chemba ya Biashara (TCCIA), Octavian Mshiu, aliiomba Serikali kuona umuhimu wa maonyesho hayo kuwa kwenye kalenda yake ili kuweza kuvutia washiriki wengi zaidi.

Alisema Tanga ni mji wa viwanda, hivyo maonyesho hayo yana lengo zuri la kutangaza bidhaa zinazozalishwa na viwanda hivyo, lakini kama yakitambulika kitaifa yataweza kuvutia watu wengi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles