30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI MPANGO AAHIDI NEEMA NALIENDELE

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Na Benny Mwaipaja, WFM, Mtwara                   |                     


WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, ameuahidi uongozi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo Naliendele kuwa Serikali itakiwezesha pamoja  na vituo vingine vya utafiti viendeleze kazi ya utafiti wa mazao ya kilimo ambacho kinategemewa na Watanzania wengi kujikwamua katika uchumi.

Dk. Mpango  alitoa ahadi hiyo jana alipotembelea Kituo cha Utafiti Naliendele mkoani Mtwara.

Uongozi wa kituo hicho ulieleza wasiwasi wake wa kupata rasilimali fedha za kuendeleza utafiti wa mazao likiwamo zao la korosho pamoja na watumishi baada ya kuondolewa   fedha za ushuru wa korosho  inayouzwa nje.

Fedha hizo zilikuwa zikitumika kuendeleza utafiti huo.

Alisema Serikali inatambua umuhimu wa shughuli za utafiti katika kuendeleza uchumi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Alisema  atajitahidi kama Waziri wa Fedha na Mipango kwa kushirikiana na waziri mwenzake anayeshughulikia kilimo,   taasisi hiyo isikwame kufanya shughuli zake.

“Niwahakikishie kabisa Serikali haitakubali utafiti wa mazao yote unaofanyika hapa, likiwamo zao la korosho udhurike, litakuwa ni janga kubwa.

“Kwa hiyo upatikanaji wa fedha za kituo hiki litakuwa ni moja ya vipaumbele vyangu,” alisema Dk. Mpango.

Alisema kilimo ndiyo uti wa mgongo wa taifa na hakutakuwa na mapinduzi ya viwanda bila kilimo, kwa sababu viwanda vinavyojengwa vinatarajiwa kuongeza thamani ya mazao ya kilimo  na mazao ya mifugo na uvuvi.

Mkurugenzi wa Kituo hicho, Dk. Omari Mponda, alisema kinahitaji zaidi ya Sh bilioni saba kwa mwaka   kiweze kuendeleza shughuli za utafiti, baada ya Serikali  kupanua shughuli za utafiti wa   korosho kwenye mikoa mingine.

Alisema hivi sasa kimeelekeza nguvu zake katika utafiti wa ugonjwa mpya unaoathiri korosho kwa kiwango kikubwa,   ujulikanao kama mnyauko fusari (Fusarium wilt).

Ugonjwa huo umeathiri zao hilo katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Mkuranga, Masasi, Tandahimba, Mtwara na Liwale.

Dk. Mponda alisema  changamoto kubwa inayowakumba ni ukosefu wa fedha za kuendeleza utafiti huo.

“Kituo hiki kina zaidi ya asilimia 50 ya watumishi ambao wameajiriwa kwa njia ya mikataba na wanahitaji kulipwa vizuri  wabaki hapa kuendeleza shughuli za utafiti.

“Ndiyo maana nasema tuna mahitaji makubwa ya fedha na tunaiomba Serikali iliangalie jambo hili,” alisema Dk. Mponda.

Kituo cha Utafiti Naliendele   mkoani Mtwara, kinatajwa kuwa ni kitovu cha utaalamu  wa zao la korosho katika Bara la Afrika.

Utafiti mwingi ukiwamo aina 54 za mbegu za   korosho unakifanya kituo hicho kuwa tegemeo kwa masuala ya utafiti katika nchi nyingi za Afrika ambazo hutumia taasisi hiyo kupata teknolojia ya uzalishaji wa mbegu bora za mazao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles