23.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuya aizika rasmi CHC

Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum
Waziri wa Fedha, wa Fedha, Saada Mkuya Salum

Na Khamis Mkotya, Dodoma

WAZIRI wa Fedha, Saada Mkuya Salum, ametangaza kulizika rasmi Shirika Hodhi la Mali za Serikali (CHC) ambalo kwa muda mrefu limezua mjadala kuhusu uhai.

Mkuya alitangaza msimamo huo wa Serikali juzi bungeni mjini hapa wakati akihitimisha mjadala wa bajeti kuu ya Serikali kwa kujibu hoja za wabunge mbalimbali.

Katika mjadala huo uliodumu kwa siku saba baadhi ya wabunge walitaka shirika hilo ambalo linapaswa kukoma Juni 30, mwaka huu liongezewe muda ili liendelee na shughuli zake.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Mkuya alisema baada ya mjadala wa muda mrefu shirika hilo sasa halina budi limalize muda wake na kueleza kuwa shughuli zake zitahamishiwa chini ya Msajili wa Hazina.

“Hili shirika limekuwamo kwa muda mrefu na limekuwa likiongezewa muda mara kwa mara, sasa limalize muda wake shughuli za shirika hilo pamoja na wafanyakazi wake wataenda kwa msajili wa hazina,” alisema.

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), ni miongoni mwa wabunge ambao walitoa hoja ya kutaka shirika hilo liongezewe muda baada ya muda wake kumalizika Juni 30.

Mpina ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi na Viwanda, alitoa hoja hiyo wakati akichangia mjadala wa bajeti kuu baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Katika mjadala huo, Mpina alisema haoni sababu shirika hilo lisipewe muda wa ziada kwa kuwa Serikali imeshindwa kuwasilisha bungeni tathimini ya kazi za shirika hilo licha ya kupewa miaka mitatu.

Wakati mbunge huyo akitaka shirika hilo liongezwe muda, wananchi wengine wakiwamo wabunge wamekuwa wakipinga shirika hilo kuongezewa muda kwa madai kuwa hakuna kinachofanywa na shirika hilo zaidi ya ulaji tu.

Moja ya majukumu ya shirika hilo ni ukusanyaji wa madeni yanayotokana na mali za Serikali pamoja na kuendesha kesi, lakini inadaiwa kuwa madeni mengi bado yapo nje licha ya uhai wake kuendea ukingoni.

“Ukomo wa CHC ni tarehe 30 mwezi huu, mwaka jana waziri wa fedha aliahidi kuwa Serikali italeta tathimini ya kazi ya shirika hilo lakini hadi sasa Serikali haijaleta tathimini hiyo kwenye kamati yetu na muda umekwisha.

“Hatutaendelea kuburuzwa kwa kuwa Serikali imeshindwa kuleta tathimini ya kazi za CHC ni vema shirika hili likaongezewa muda hata kama ni mwaka mmoja wakati tukiendelea kusubiri tathimini ya Serikali,” alisema.

Akizungumzia madeni ya wazabuni na wakandarasi, Mpina alisema Serikali imetangaza kuwa itaanza kulipa madeni hayo lakini haijaonyesha ni kwa namna gani fedha hizo zitalipwa.

“Madeni ya wakandarasi na wazabuni sasa yamefikia Sh trilioni 1.3, Serikali inasema inahakiki madeni na yataanza kulipwa katika bajeti hii hakuna fedha zilizotengwa kwa ajili madeni hayo hizo fedha zitalipwa kutoka wapi,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Mpina alisema Serikali imewageuka wananchi huku akiitaka Serikali ilipe madeni hayo kabla bajeti hiyo haijafikiwa ukomo wa kupitishwa.

Katika kipindi hicho cha mjadala aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, aliibua sakata la uuzwaji wa kiwanja cha shirika hilo kilichopo Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam huku akikanusha kuhusika katika mpango huo.

Mkulo alisema kiwanja hicho kiliuzwa kihuni na kueleza kuwa sakata la kiwanja hicho ni bomu kuliko Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) lilivyouzwa.

Mkulo ambaye ni Mbunge wa Kilosa, alisema hakuhusika na uuzwaji wa kiwanja hicho ambacho kwa mara ya kwanza alitajwa bungeni kuwa yeye ndiye mhusika mkuu na mwizi namba moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles