22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 28, 2021

Waziri Mkuu wa Ivory Coast afariki dunia baada ya mkutano wa Baraza la Mawaziri

Alikuwa mgombea urais wa chama tawala uchaguzi wa Oktoba, sasa Rais Ouattara ashinikizwa kuwania muhula wa tatu

 ABIDJAN, IVORY COAST

WAZIRI Mkuu wa Ivory Coast, Amadou Coulibaly amefariki dunia juzi baada ya kuugua wakati wa kikao cha Baraza la Mawaziri.

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 61 alikuwa amechaguliwa kuwa mgombea wa chama tawala cha RHDP katika uchaguzi wa mwezi Oktoba, baada ya Rais Alessane Ouattara kusema kuwa hatowania muhula wa tatu.

Coulibaly alikuwa amerudi kutoka Ufaransa ambako alipatiwa matibabu ya moyo kwa miezi miwili.

Rais Ouattara alisema kwamba Coulibaly alianza kuhisi vibaya wakati wa kikao cha kila wiki cha Baraza la Mawaziri na akapelekwa hospitali ambako alifariki baadaye.

Coulibaly alifanyiwa upandikizaji wa moyo mwaka 2012 na Mei 2 mwaka huu alikwenda Ufaransa kuwekewa bomba katika mshipa wake wa damu na alirudi katikati ya wiki iliyopita.

“Nimerudi kuchukua mahala pangu kando ya rais ili kuendelea na jukumu la kujenga taifa letu,” alisema mara baada ya kuwasili kutoka Ufaransa.

Taarifa moja katika gazeti la Le Monde Jumatatu iliyopita ilimnukuu ofisa mmoja wa kigeni ambaye yupo nchini hapa kama mchunguzaji wa uchaguzi huo akisema; “Iwapo Gon Coulibaly hajapona, Ouattara atakuwa hana chaguo bali kuwania kwa muhula mwengine kwa sababu hakuna mpango mwengine.”

Tayari viongozi wa chama tawala wamekubaliana kumshinikiza Rais Ouattara kuwania muhula wa tatu wa urais katika uchaguzi wa Oktoba baada ya kifo cha Coulibaly.

Machi mwaka huu, Ouattara alitangaza kuwa hatowania tena urais baada ya miaka 10 ofisini na tayari alikuwa amemteua Coulibaly kuwa mgombea wa chama chake katika uchaguzi mkuu.

Ouattara ambaye alizusha wasiwasi wa muda mrefu kuhusu hatma yake ya kisiasa, alitangaza kwamba hatowania muhula wa tatu wa urais.

‘’Nawatangazia rasmi kwamba ninachukuwa hatua ya kutokuwa mgombea katika uchaguzi wa rais wa Oktoba 31, 2020 na kukabidhi madaraka kwa kizazi kipya,’’ alisema Ouattara mbele ya wabunge na maseneta waliokusanyika kwenye kikao maalumu mjini Yamoussoukro, mji mkuu wa nchi. Kauli hiyo iliyotolewa katika hotuba yake ya dakika zaidi ya thelathini, ilipokewa kwa makofi na vigelegele vya wabunge na wanafunzi wa shule za sekondari na chuo kikuu walioalikwa.

‘’Presi, Presi, Merci, Merci’’ (Rais, rais, asante, asante) walikuwa wakiimba wanafunzi hao.

‘’Tunafurahi sana na hatua yake ya kuwaachia madaraka vijana. Ni mtu anayeheshimu kauli yake. Ninafurahia sana kauli hiyo ya rais japokuwa mimi sio mfuasi wake,’’ alisema Daouda Bakayoko, ambaye ni mwanafunzi wa sekondari mjini Yamoussoukro.

Ouattara, mwenye umri wa miaka 78 alichaguliwa kwa mihula miwili mwaka 2010 na 2015.

Kifo cha Coulibaly kilichotokea chini ya wiki moja tangu aliporejea kutoka mapumziko ya kimatibabu nchini Ufaransa, kimekiacha chama cha RHDP kikihaha kupata mgombea mwingine.

Muda wa mwisho wa kuwasilisha jina la mgombea wa urais ni Julai 31.

Uchaguzi huo wa Oktoba unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa tangu mwaka 2010 baada ya ushindi wa Ouattara dhidi ya Laurent Gbagbo, ushindi uliochochea vita vilivyosababisha vifo vya watu 3,000.

Kukaribia kwa uchaguzi wa Oktoba kunazorotesha hali ya kisiasa nchini hapa, miaka 10 baada ya vurugu hizo za baada ya uchaguzi wa 2010 hadi 2011. 

Uchaguzi wa Serikali za mitaa na madiwani wa 2018 pia uligubikwa na wizi wa kura na umwagikaji wa damu.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,502FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles