Na Mwandishi Wetu-GAIRO
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema atatuma mkaguzi aende kuchunguza hali ya upatikanaji wa dawa kwenye zahanati na kituo cha afya cha mjini Gairo, mkoani Morogoro.
Kauli hiyo aliitoa jana wakati akiwahutubia wakazi wa mji wa Gairo na vitongoji vyake kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Gairo ‘A’.
Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya kumhoji Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dk. Albert Lyaruu kama anamiliki duka la dawa au laa na kujibiwa kwamba hana duka la dawa ingawa alikiri kwamba baadhi ya watumishi wa idara yake wanayo maduka ya dawa.
“Sasa ni lazima nilete mkaguzi kutoka ofisi yangu ili tupate picha halisi kama dawa zinazoletwa zinafika, na kama zinafika zinatumikaje. Huyu mkaguzi atakuja kukukagua wewe mwenyewe na kwenye zahanati zako.
“Kwenye mkutano wangu na watumishi wa Serikali nimewaeleza kwamba ninyi ni desk officers (maofisa wa kukaa ofisini tu), wala hamuendi vijijini kuona hali halisi ikoje. Ndiyo maana wananchi hawa wanalalamikia kukosa dawa na wewe wala hujui,” alisema Majaliwa.
Pamoja na hali hiyo alimtaka mganga huyo kuhakikisha anakwenda kwenye vituo vya afya na zahanati ili kuangalia matumizi ya dawa na kama hatofanya hivyo anaweza kupata kesi kama ya Mkoa wa Shinyanga ambapo mganga wa kituo cha afya alikutwa na dawa za Serikali nyumbani kwake, baada ya wanachi kumwekea mtego hadi akakamatwa.
“Serikali haizuii watumishi kuwa na maduka ya dawa, tunachokataa sisi ni kuchukua dawa za Serikali ambazo zinatakiwa kuwatibu wananchi na kuzipeleka kwenye maduka yenu. Tumezuia pia kuwepo kwa maduka ya watu binafsi nje ya hospitali, zahanati au kituo cha afya,” alisema
Waziri Mkuu aliwataka wananchi wa Gairo wawe macho na walinde mali za umma na inapobidi watoe taarifa mara tu wanapobaini kuna mtu anatumia mali ya umma vibaya.
Waziri Mkuu alikuwa alimwita jukwaani, Dk. Lyaruu ili aeleze ni kiasi gani cha fedha amepokea kutoka Serikalini kwa ajili ya ununuzi wa dawa na alipotoa mchanganuo wake, wananchi waliohudhuria mkutano huo walizomea na kudai kuwa siyo kweli.
“Ninapokea shilingi milioni 109 kila robo mwaka. Na katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho tumepokea shilingi milioni 109 na kati ya hizo tunatoa asilimia 33 ambazo ni sawa na shilingi milioni 36 kununua dawa na vifaa tiba. Kwa hiyo hadi sasa hali ya dawa ni nzuri na upatikanaji wake ni kati ya asilimia 85 hadi 90,” alisema Dk. Lyaruu.
Kutokana na majibu yake hayo, wananchi walimzomea daktari huyo na kudai kuwa wananunua dawa hizo kwenye maduka ya dawa.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi waliohudhuria mkutano huo kwamba dawa zinazopatikana kwenye zahanati zinatofautiana na dawa zinazopelekwa kwenye kituo cha afya, hospitali ya wilaya au ya mkoa.