Na SARAH MOSES, DODOMA
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa anatarajiwa kuhamia rasmi mkoani Dodoma baada ya kumalizika   vikao vya bunge, imeelezwa.
Vikao hivyo  vinatarajiwa kuanza Septemba sita na kumalizika baada ya wiki mbili tofauti na ilivyotarajiwa kuwa angehamia mjini hapa juzi (Septemba mosi mwaka huu).
Hayo yaliezwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana alipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuhusu  maandalizi ya kumpokea Waziri Mkuu.
Rugimbana alisema kutokana na utamaduni katika Mkoa wa Dodoma kunapokuwapo   vikao vya bunge, mara nyingi hazifanyiki shughuli mbalimbali ambazo zinaonekana kuwa na mikusanyiko ya watu.
Alisema kwa sababu hiyo,  uongozi wa mkoa ulimuomba Waziri mkuu akubali kuhamia rasmi   Dodoma baada ya kumalizika  vikao vya bunge.
Rugimbana alisema hatua hiyo ya kumuomba Waziri mkuu kuhamia Dodoma baada ya kumalizika   vikao vya Bunge kunatokana na kuwapa nafasi wananchi  kupata muda wa kumlaki ikiwa ni pamoja na  kuhudhuria kwa wingi katika mkutano ambao Waziri Mkuu ataweza kuufanya   kujitambulisha.
Alisema kwa sasa mkoani Dodoma, maandalizi ya serikali kuhamia hapa yamekamilika kwa asilimia 90.
Kila kitu kipo tayari na hakuna wasiwasi wowote katika kuwapokea wageni ambao wanatarajiwa kufika mjini hapa, alisema.
Alisema kwa sasa mji umepangwa katika hali ambayo haitaweza kusababisha kuwapo  msongamano wa watu  na magari.
RC alisema limetengwa eneo la zaidi ya hekta 200 ambalo litajengwa kwa ajili ya wajasiriamali  wadogo ambalo lipo   Zuzu nje kidogo ya mji.
Alisema lengo ni kutenga eneo hilo ni kuwafanya wananchi kujua ni bidhaa gani zinaweza kupatikana eneo Fulani.