26.1 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu awataka watanzania kutoa taarifa ya bidhaa zisizo rasmi

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watanzania watoe taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapokuta bidhaa zisizo rasmi zimeagizwa kutoka nje, zinazalishwa au zinasambazwa nchini.

Ametoa wito huo Bungeni leo Agosti 29, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Saasisha Mafue kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani ili kudhibiti tabia ya vijana kulewa sana nyakati za mchana hali ambayo inasababishwa na uingizaji holela wa pombe kali.

“Serikali inao utaratibu wa kutambua uzalishaji na uingizaji wa vileo nchini ambao unadhibitiwa kwa kutoa vibali vya biashara kwa wasambazaji. Vilevile inaendelea kutoa elimu juu ya madhara ya ulevi kupitiliza ili kuwalinda vijana wetu.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuwahamasisha vijana wajiunge kwenye vikundi ili wafanye shughuli za ujasiriamali. Utaratibu huo umesaidia vijana wetu kupata kipato chao binafsi na familia zao.

Ili kudhibiti hali hiyo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kutoa elimu ili vijana wengi waingie kwenye shughuli za ujasiriamali na kuimarisha sheria za waagizaji, wauzaji na wasambazaji ili kuhakikisha kila kinachoingizwa nchini kinakidhi mahitaji ya afya ya Watanzania.

“Jamii itusaidie kutambua utengenezaji wa bidhaa usiokuwa rasmi ambao haujapata vibali rasmi kwani unachangia kutengeneza bidhaa zenye vileo vikali. Nitoe wito kwa taasisi zote zinazojihusisha na masuala ya vijana ziendelee kutoa elimu ya ujasiriamali, kuwafundisha maadili mema vijana wetu na kuwapa stadi za maisha.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema kuwa huduma za afya nchini zimeimarishwa sana na uwekezaji mkubwa umefanywa kiasi kwamba hatua za awali za utambuzi wa mama mjamzito zinaweza kubaini aina ya ulemavu kwa mtoto aliyenaye tumboni.

“Tafiti zetu za Wizara ya Afya zinaonesha kuwa hatua za awali zinaweza kubaini ulemavu na kuna uwezekano mkubwa wa kupunguza ulemavu kwa zaidi ya asilimia 80. Kwa maana hiyo, uwekezaji uliofanywa kuanzia ngazi ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, za mkoa, za kanda na Taifa si tu kuamua hospitali moja katika mkoa iwe inatoa huduma kwa walemavu bali kwenye vituo vyote ambavyo Serikali imeviboresha.”

Ametoa wito kwa akinamama wahudhurie kliniki mapema ili wapate elimu na kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara hadi atapojifungua.

Alikuwa akijibu swali la Khadija Taya (Viti Maalum) ambaye alitaka kujua ni upi mkakati wa Serikali wa kuweka vituo katika kila mkoa ambavyo vitatoa huduma za kunyoosha viungo kwa watoto wanaozaliwa na ulemavu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles