24.7 C
Dar es Salaam
Thursday, September 12, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu awataka wakuu wa taasisi kuwapa posho madereva

Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa taasisi wahakikishe kuwa madereva wao wanapatiwa stahiki zao ikiwemo posho za safari, sare za kazi na mafunzo wawapo kazini.

“Wakuu wa taasisi hakikisheni madereva wanapata stahiki zao kikamilifu kwa kuzingatia sheria. Ni muhimu posho ya kujikimu nje ya vituo za safari zilipwe kulingana na siku za safari na stahiki za wahusika wenyewe. Posho za sare zitolewe kwa wakati ili wawe smart,”

Ametoa wito huo Agosti 20, 2024 wakati akifungua Kongamano la siku tano la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania (CMST) kwenye kituo cha mikutano cha kimataifa (AICC) jijini Arusha.

Waziri Mkuu amesema madereva hawana budi kuandaliwa mafunzo kazini na waajiri wao na kulipiwa gharama husika ili kuboresha umakini na utendaji kwa kuzingatia mabadiliko mbalimbali ya kiteknolojia.

Amesema waajiri waangalie utaratibu wa kazi za madereva wao na bila kuathiri utekelezaji wa majukumu, wawawekee ratiba zinazowawezesha kupata muda wa kupumzika.

Amewataka madereva wa Serikali wawe mfano wa kuigwa kwa madereva wote kwa kuzingatia majukumu yao kwa umakini na kwa heshima; watunze vyombo vyao vya usafiri na washirikiane na timu za matengenezo ili kuhakikisha kuwa magari ya Serikali yanaendelea kuwa katika hali bora ya kuendeshwa.

Kuhusu usalama na utunzaji wa siri, Waziri Mkuu amewataka madereva wazingatie suala hilo kwa kutunza nyaraka za ofisi na kuhakikisha mazungumzo wanayoyasikia wakiwa katika majukumu yao hayafiki kwa wasiohusika.

Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa kwenye risala yao zikiwemo za uchache wa madereva wanawake Serikalini, Waziri Mkuu amewasihi wanawake wote wenye sifa stahiki wahakikishe wanaomba fursa za udereva zinapotangazwa na kwa wale wenaopenda kazi ya udereva wajitokeze kwenda kujifunza kupitia vyuo mbalimbali vya umma na binasfi ili wawe na sifa stahiki.

“Serikali itaendelea kuwapa kipaumbele katika ajira wenye sifa kadri ya nafasi za ajira zinapotangazwa. Nitoe rai kwa jamii kuhamasisha watoto wa kike kupenda na kujiunga na masomo ya udereva kwani ni fani ambayo wanawake wanaifanya kwa ufanisi mkubwa sana,”amesema.

Kuhusu malipo kwa madereva wa darasa la saba ambao waliondolewa kwenye zoezi la uhakiki wa vyeti, Waziri Mkuu amesema hadi kufikia Juni, 2024, Mifuko ya Pensheni imepokea jumla ya madai 15,022 ya watumishi walioondolewa kazini kwa sababu ya vyeti kutoka kwa waajiri mbalimbali.

“Kati ya hayo, madai 14,982 sawa na asilimia 99.73 yenye jumla ya shilingi bilioni 45.67 yemehakikiwa na kulipwa. Nitumie fursa hii kutoa rai kwa wote ambao wana stahili ya kulipwa kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali wawasilishe madai yao kupitia fomu iliyojazwa na mwajiri kwenye Mfuko husika ili hatua stahiki zichukuliwe.

Akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema tangu Mei 2023, Wizara hiyo imewasaidia madereva hao kwa kuondoa kikwazo cha ‘Trade Test’ ambacho kilikuwa kinatumika kama kigezo kikuu cha kuwapandisha madaraja.

Amesema wizara hiyo imekuwa ikitoa ushauri kwa Chama hicho kiimarishe uhusiano na vyama vingine vya kitaaluma kama vile TAPSEA (Makatibu Muhtasi) na TRAMPA (Masjala) kama njia ya kukuza mahusiano chini ya dira za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Naye Mwenyekiti wa Chama hicho, Flora Myandavile, amesema kwa mwaka huu washiriki wa kongamano hilo wamefikai 1,310 ambapo 1,200 wanatoka Tanzania Bara na 110 wanatoka Tanzania Visiwani.

Amesema chama hicho kina wanachama 7,241 nchi nzima na kwamba kati ya hao, 7,191 ni wanaume na 50 ni wanawake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles