29.4 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

WAZIRI MKUU  AWAPONGEZA NSSF, PPF UJENZI  KIWANDA CHA SUKARI

Na Mwandishi Wetu-MOROGORO


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amepongeza hatua ya mifuko ya hifadhi ya jamii hapa nchini kuwekeza kwenye sekta ya viwanda, huku akitoa wito kwa jamii, hususani vijana, kuhakikisha wanaonyesha uzalendo kwa kujitolea kwa vitendo kuunga mkono jitihada zinazolenga kutatua tatizo la ajira na kuinua uchumi wa taifa.

Pongezi hizo alizitoa mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro, baada ya kuongoza kazi ya upandaji wa miwa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono mradi mkubwa wa ujenzi wa kiwanda cha sukari unaofahamika kama Mkulazi II, unaotekelezwa kwa ubia kati ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya NSSF na PPF kupitia Kampuni Hodhi ya Mkulazi Holding katika Gereza la Mbigiri, Dakawa mkoani hapa.

“Pamoja na kutoa pongezi kwa mifuko yetu ya hifadhi ya jamii hapa nchini kwa kuitikia vema wito wa Serikali ya Awamu ya Tano katika uwekezaji wa viwanda vyenye tija kwa taifa, kipekee nitoe wito kwa jamii, hususani vijana, kuhakikisha wanaunga mkono jitihada hizi kwa kujitolea ujuzi na maarifa katika kufanikisha azma hii ya Serikali inayolenga kuwanasua kutoka kwenye uhaba wa ajira.

“Vijana hawa ambao kwa sasa wamepatiwa maturubai ya kujihifadhi, wamekuwa mfano wa kuigwa na wenzao nchi nzima na nitazifikisha salamu zao kwa mheshimiwa rais ajue jitihada zake zinatafsiriwa vyema sana na vijana wazalendo wa taifa hili,” alisema.

Akizungumzia mradi huo, Waziri Mkuu alisema pamoja na kumaliza tatizo la uhaba wa sukari hapa nchini, pia utapunguza tatizo la ajira sambamba na kukuza uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Kazi, Ajira, Sera, Bunge, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema mifuko ya hifadhi ya jamii kwa sasa inatekeleza miradi ya viwanda ipatayo 28 ambayo ipo katika hatua mbalimbali.

Naye Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Phillip Mpango, aliahidi kwenda kutoa maelekezo kwa Benki ya Kilimo nchini kuhakikisha inafika maeneo yote ya mradi huo.

Huku Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha taifa linazalisha sukari tani milioni mbili ili lijitosheleze na kuuza nje ya nchi. Kwa sasa licha ya mahitaji ya sukari kuwa ni tani 600,000 taifa linazalisha tani takribani laki tatu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mkulazi ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Pensheni wa PPF, William Erio, waliihakikishia Serikali, wanachama na wadau wote wa mifuko hiyo kuwa utekelezaji wa mpango huo umelenga kuongeza ajira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,504FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles