28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri mkuu atoa maagizo chuo cha ulinzi

Brighiter Masaki, Dar es Salaam

WAZIRI Mkuu  wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi wa Chuo cha Ulinzi cha Taifa uweke malengo endelevu yatakayokifanya kiwe kituo bora, bobezi,  kitakachotegemewa katika ulinzi, usalama na mikakati.

Majaliwa ametoa wito huo leo Alhamisi, Julai 22, 2021 katika mahafali ya tisa katika kozi ya usalama na mikakati ya Chuo Cha Taifa cha Ulinzi (NDC), kilichopo Kunduchi, Dar Es Salaam.

Amesema Serikali  itahakikisha chuo hicho kinakuwa ni kituo cha ufahari katika kutoa elimu ya juu kwa maafisa, watendaji kutoka vyombo vya ulinzi na usalama na watumishi wa umma.

Waziri Majaliwa, ameongeza kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa chuo hicho katika kutoa mafunzo yanayowajengea uwezo viongozi na watendaji mbalimbali kwenye masuala ya usalama na mikakati.

“Hadi sasa maafisa waandamizi 300 kutoka vyombo vya ulinzi na usalama ndani na nje ya nchi na wengine kutoka katika taasisi za umma za kiraia wamenufaika na programu hii inayotolewa na chuo cha Taifa cha Ulinzi,” amesema

Amesema kuwa chuo hiko kimeendelea kuwa sehemu muhimu katika kujenga na kuimarisha mahusiano ya mtu mmoja mmoja kwa washiriki wa program zake sanjari na kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kimataifa kwa maslahi mapana ya nchi yetu.

Waziri mkuu pia amekitaka chuo hicho kihakikishe kuwa kinatoa mafunzo na utaalamu ambao utasaidia katika kukabiliana na matishio ya kiusalama ya karne ya 21 vikiwamo vitendo vya kigaidi, usafirishaji haramu wa binadamu, dawa za kulevya, uhalifu wa kimtandao na janga la UVIKO-19.

Aidha, Waziri Mkuu amezishukuru nchi washiriki kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho  na amewahimiza waendelee kuwaleta maafisa wao waandamizi kupata mafunzo kupitia chuo hicho.

“Nimefarijika kuwaona baadhi ya wahitimu wa programu hii kutoka nchi rafiki za Bangladesh, Burundi, Kenya, Nigeria, Malawi, Uganda na Zambia. Uwepo wenu ni kielelezo tosha cha imani mliyonayo kwetu hususani katika kuhakikisha viwango vya ubora vya chuo hiki vinasimamiwa ipasavyo,” amesema Waziri Majaliwa.

Naye Kansela wa chuo hicho, Balozi Marten Lumbanga, amesema kuwa wataendelea kusimamia ubora wa masomo yanayotolewa chuoni hapo ili kukifanya chuo hicho kuwa na hadhi ya kimataifa katika utoaji wa elimu bora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,307FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles