WAZIRI MKUU ATANGAZA VITA NA ‘WAKWARE’

0
497

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi, wazazi wa mwanafunzi waliopokea mahari, wazazi ambao walimsindikiza mwanaume kuoa mwanafunzi na wazazi wa mwanafunzi atakayeolewa watafungwa jela miaka 30.

Waziri ametoa agizo hilo jana wakati akizungumza na viongozi, walimu na wanafunzi wa shule za sekondari wanaosoma masomo ya sayansi, waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa usambazji wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari Tanzania bara, iliyofanyika viwanja vya Lugalo Jeshini, Dar es Salaam.

Alisema Serikali itahakikisha inasimamia sheria hiyo kisawa sawa kwa lengo la mtoto wa kike apate elimu iliyo sawa kama wengine.

Pia aliwataka watoto wa kike kusoma kwa bidii na kuacha vishawishi vitakavyowarudisha nyuma katika masomo yao.

“Watoto wa kike mnatakiwa na ninyi mjichunge, achaneni na vishawishi, mtu anapita anakusalimia mara tatu au anakwambia njoo nyumbani nikufundishe, achana naye, mwambie mwalimu wangu yupo atanifundisha,’’ alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu Majaliwa alizindua usambazaji wa vifaa vya maabara vyenye thamani ya Sh bilioni 16.9, vitakavyosambazwa katika kanda 11 za kielimu.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema ununuzi wa vifaa hivyo umegharimu Sh bilioni 16.9 kutokana na michango ya washirika wa maendeleo kutoka Benki ya Dunia, Shirika la Misaada ya Maendeleo la Kimataifa (DfID) na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Sweden (CIDA).

Alisema usambazaji wa vifaa hivyo utafanyika kwenye kanda 11 za kielimu na utahusisha shule za wananchi 1,625 na shule kongwe 71.

 “Wizara ya Elimu imenunua vifaa hivyo chini ya programu ya Lipa Kulingana na Matokeo. Vifaa hivi vinakidhi ufundishaji kwa vitendo kwa asilimia 100 kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita,” alisema.

Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania litahakikisha linavisambaza vifaa hivyo katika kanda zote 11 zilizoteuliwa.

Akifafanua kuhusu maghala ya jeshi kutumika kutunzia vifaa hivyo na kemikali, Dk. Mwinyi alisema Serikali imepata unafuu mkubwa kwa kutumia maghala hayo na hivyo kuokoa fedha ambazo zingetumika kulipia sehemu nyingine.

Kwa upande wake, mshauri wa elimu kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza (DFID), Tanya Zebroff, alisema wamefurahi kupata fursa ya kuisaidia Serikali ya Tanzania na watoto katika suala la elimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here