22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI MKUU ARIDHISHWA UWEKEZAJI SAGCOT

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa

Na Mwandishi Wetu-IRINGA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amempongeza mdau wa Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT) kwa upande wa ufugaji, ASAS Diaries Ltd kwa kuwainua wafugaji wadogo wadogo mkoani Iringa.

Hayo aliyasema jana mjini hapa, alipotembelea shamba kubwa la mifugo linalomilikiwa na ASAS, huku akiwataka wawekezaji wengine nchini kuiga mfano wa mwekezaji huyo kwani itasaidia kupunguza migogoro isiyo ya lazima.

“Huu ni mfano mzuri wa uwekezaji ambao unasaidia wafugaji wadogo wadogo wanaomzunguka mwekezaji mkubwa kunufaika kwa soko la uhakika, utaalamu na huduma za kijamii pia,” alisema Majaliwa.

Mbali na hilo, Waziri Mkuu alijionea ufugaji mkubwa wa kisasa katika shamba hilo ambalo lina ng’ombe wa kisasa wa maziwa zaidi ya 1,000 na kuwataka wafugaji wadogo kuchangamkia fursa wanazozipata.

“Wakati sasa umefika kwa Watanzania kupenda bidhaa zinazotengenezwa hapa nyumbani kwani zipo zenye ubora wa hali ya juu,” alisema Waziri Mkuu.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mtendaji wa ASAS Diaries Ltd, Fuad Jaffer, alisema kampuni hiyo  imefanikiwa katika uboreshaji wa mifugo, udhibiti wa magonjwa ya mifugo, kuzalisha mitamba na madume bora.

“Tumefanikiwa kuimarisha mahusiano mazuri na jamii kwani kampuni imeajiri watumishi wengi kutoka maeneo yanayotuzunguka,” alisema Jaffer.

Alimwambia Waziri Mkuu kuwa kiwanda kinasindika lita 14,000 za maziwa kila siku ambayo ni sawa na asilimia 24 ya uwezo wake.

Majaliwa alitembelea shamba hilo la ASAS ambaye pia ni mdau muhimu wa SAGCOT, akiwa njiani kuelekea Mkoa wa Njombe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kongani na Ubia wa Maendeleo wa SAGCOT, Maria Ijumba, alisema kuwa ASAS ni mfano wa kuigwa kwa wadau wa SAGCOT kwenye sekta ya ufugaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles