Waziri Mkuu apiga marufuku vikundi vya ulinzi wakati wa kampeni

0
1181

Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepiga marufuku vikundi vya ulinzi wa jadi, ulinzi binafsi au vya mashabiki wa vyama vya siasa kutumika kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni zitakazoanza Novemba 17 hadi 23, mwaka huu au maeneo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Waziri Mkuu ametoa onyo hilo jana wakati akizindua wiki ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasioambukiza sambamba na mpango wa taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza. 

“Vyombo vya ulinzi na usalama hususani Jeshi la Polisi, Mgambo wenye sare na maofisa wanaosimamia ulinzi vitatumika kuhakikisha kunakuwepo na utulivu wakati wote wa kampeni na uchaguzi,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura na Serikali imejipanga vya kutosha kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.

Pamoja na mambo mengine,Waziri Mkuu amewataka wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na kubadili tabia na mwenendo wao wa ulaji wa vyakula kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga, matunda.

“Kila mtu ana wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama sigara na pombe, kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi au shughuli za nguvu, kuzingatia mlo unaofaa hasa kwa kuondoa au kupunguza chumvi, sukari na mafuta. Tujipange kukabiliana na madhara mengine yatokanayo na uharibifu wa mazingira na tabianchi,” amesema. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here