WAZIRI MKUU AKABIDHI MAGARI YA WAGONJWA

0
503

Na Mwandishi Wetu-RUANGWA


WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amefanya ziara katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa na kukabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa.

Amesema kati ya magari hayo, moja ni kwa hospitali hiyo ya wilaya na la pili litapelekwa katika Kituo cha Afya cha Mandawa.

Alikabidhi magari hayo jana alipotembelea hospitali hiyo, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi mkoani Lindi.

Alisema magari hayo ni mwendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi wake.

“Rais wetu Dk. John Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono,” alisema.

Waziri Mkuu alisema magari hayo ya kisasa yatasaidia kurahisisha usafiri kwa  wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura katika hospitali kubwa.

Kabla ya kukabidhi magari hayo, Waziri Mkuu alitembelea wodi ya akina mama na ya  watoto waliolazwa katika hospitali hiyo na akasema kwamba ameridhishwa na hali ya utoaji huduma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Rashid Nakumbya, alisema magari hayo ni faraja kwao kwa kuwa walikuwa na changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wa dharura.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here