27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu ahimiza mshikamano kwa Watanzania

Mwandishi wetu-Lindi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania waendelee kushikamana na wazingatie ujumbe wa mbio za Mwenge unaohimiza umuhimu wa maji, uchaguzi wa Serikali za Mitaa, vita dhidi ya rushwa, malaria, Ukimwi na dawa za kulevya.

Alitoa wito huo jana wakati akizungumza na viongozi wa halmashauri za Lindi na Ruangwa na wananchi wa Kijiji cha Nangumbu, Uwanja wa Shule ya Msingi Nangumbu ambako mwenge ulipokewa ukitokea Nyangao wilayani Lindi.

Majaliwa ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa, aliwasili wilayani humo juzi jioni kushiriki mbio za mwenge.

Leo mwenge huo utaelekea Nachingwea, kesho  utaenda Liwale, Jumamosi Kilwa na Jumapili utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na kuzimwa Oktoba 14.

Majaliwa aliwataka wananchi wote wajiandikishe kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili Tanzania iweze kupata viongozi bora.

 “Tuitikie kaulimbiu ya mwaka huu kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Hapa Ruangwa, hadi jana jioni watu 28,000 walikuwa tayari wamejiandikisha. Tukachague viongozi wachapakazi na waadilifu watakaoleta maendeleo kwa nchi yetu,” alisema.

Mapema, akizungumza baada ya kupokea mwenge huo, Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa alisema utakimbizwa katika kata saba na vijiji 17 huku miradi mitatu mikubwa ya Sh bilioni 2.9 itazinduliwa.

Katika Kijiji cha Nangumbu, mwenge ulizindua mradi wa mabweni na klabu ya kupiga vita rushwa kwenye Shule ye Sekondari Hawa Mchopa. Ukiwa njiani, ulipitishwa Kijiji cha Nandagala ambako Waziri Mkuu alizaliwa.

Pia aliupokea na kuukimbiza kidogo akiwa na wanakijiji wenzake, kisha ukaendelea kukimbizwa kuelekea Kata ya Likunja ambako watazindua mradi wa maji wa Kitandi.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa mbio za mwenge wilayani Ruangwa, kiongozi wa mbio za mwenge Mzee Ali Mkongea alimshukuru Majaliwa kwa kujumuika na wananchi kushiriki ratiba ya mapokezi ya mwenge wilayani humo.

Alisema Serikali ya awamu ya tano, ndani ya miaka mitatu  imekamilisha kwa wakati miradi 124 ya maji na aliitaja baadhi yake kuwa ni miradi mikubwa ya Chalinze, Bagamoyo, Arusha, Tabora na Musoma.

Pia alisema Serikali imeendelea na uchimbaji wa visima virefu na vifupi vya maji kwa gharama ya Sh bilioni 14.

 “Serikali imeingia mkataba na Serikali ya India wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji kwenye miji 28 ya Tanzania.

“Lakini kuna changamoto nyingi kwenye miradi hii, ikiwemo matumizi mabaya ya fedha za umma na wakandarasi kujenga baadhi ya miradi chini ya kiwango.

 “Pia kumekuwa na shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji.

“Wananchi tusaidiane kuvilinda vyanzo hivi kwa sababu kazi ya kuvitunza si ya Serikali peke yake bali inaanza na mimi na wewe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles