26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI MKUU AAGIZA VIONGOZI TISA WAKAMATWE

NA MWANDISHI WETU DAR ES SALAAM


 WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amemwagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule, awakamate viongozi wa Chama cha Msingi cha Mkombozi kwa upotevu wa Dola za Marekani 21,000 ambazo ni sawa Sh milioni 47.6 za chama hicho.

Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa Kijiji cha Kangeme, Kata ya Ulowa katika Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama ambako alikwenda kuzindua mpango wa ushirika afya na NHIF.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo, baada ya kuwaita viongozi wa chama cha Mkombozi watoke hadharani na kubaini kuwa hakuwepo hata mmoja. Inadaiwa kwamba walitoroka baada ya wananchi kuanza kuzomea.

“Wabebe hawa watu, wahoji waseme hiyo fedha iko wapi na jambo la kwanza wailete hiyo fedha ya wakulima. Wakishindwa kurejesha fedha, wawekwe ndani,” alisema.

Kamanda Haule, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mwenyekiti Shilinde Abdallah na mhasibu wa chama hicho, Kulwa Shinzi pamoja na wajumbe saba wa bodi ya chama hicho.

Akiwa katika tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Kahama (KACU), Emmanuel Cherehani, alisoma taarifa ya chama na alipotaja bei ya tumbaku kuwa ni nzuri, wananchi walimzomea kupinga kile alichokisema.

Akitoa ufafanuzi kuhusu kadhia hiyo, Waziri wa Kilimo, Dk. Charles Tizeba, alisema kuna tatizo katika uteuzi (grading) wa zao hilo kwani wakulima wanalima tumbaku nzuri, lakini katika upangaji bei, wanalipwa bei ndogo.

“Kuna wakulima wanakidai Chama cha Mkombozi kiasi cha Dola za Marekani ambayo ni madai ya tumbaku waliyoiuza tangu mwaka 2014,” alisema.

Akizungumza na wananchi hao, Waziri Mkuu alisema Serikali imeamua kufufua ushirika kwa sababu ndiyo mkombozi wa wakulima.

“Tumeamua kurudisha ushirika aminifu kwa wakulima, na nirudie kutoa onyo kwa viongozi waliopata dhamana ya kuongoza ushirika wasidhani kule wameenda kupata ulaji.

“Tunataka ushirika unaosimamiwa na viongozi waaminifu. Kwenye ushirika kuna fedha na kuna mali za chama, kwahiyo ni lazima tupate viongozi ambao ni waaminifu.

“Kwa mfano, hapa Ulowa wakulima wamekuwa wakilalamikia kupewa bei ya chini wakati wao viongozi wanabeba kile cha juu na kuwaumiza wakulima. Kiongozi wa KACU kasoma taarifa hapa mkaanza kuzomea, hiyo ni dalili tosha kwamba kuna tatizo la msingi,” alisema.

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaasa wakulima waachane na tabia ya kukopa pembejeo na kufunga mikataba na makampuni ya ununuzi wa tumbaku na badala yake wajiwekee akiba ili msimu wa kilimo ukianza wasirudie tena kukopa.

“Gharama za kulima ekari moja, kuweka dawa, palizi na kuchoma haizidi Sh 150,000. Wewe amua unaweka kulima ekari ngapi, weka fedha zako kwenye akaunti usubiri msimu ujao. Kwenye hii biashara ya tumbaku, ukitafuta mikopo utabakia kuwa masikini kwa sababu huna nguvu ya kubishania bei. Wenzenu wanaolima korosho, wameacha kukopa na bei mnazisikia kila mwaka zinapanda.

“Ukiwa na mazao yako utaweza kubishana na mnunuzi. Tanzania bei ya tumbaku iko chini sababu wakulima mmetufikisha hapo kwa kupitia mikopo na mikataba na makampuni ya ununuzi. Kuanzia sasa badilikeni, ili muweze kuinua bei ya zao hili muhimu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles