23.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mhagama akabidhi Ofisi kwa waziri Lukuvi

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, katika maeneo ambayo atahitaji msaada wakati wa kuratibu shughuli za serikali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu.

Jenista alitoa ahadi hiyo leo, Agosti 20, 2024, jijini Dodoma wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) kwa William Lukuvi, aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo.

Katika hotuba yake, Waziri Mhagama aliwashukuru watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), pamoja na watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano mkubwa waliompa wakati alipokuwa akihudumu katika Ofisi hiyo.

“Nawashukuru kwa dhati watumishi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Watumishi wa Ofisi Binafsi ya Waziri Mkuu na Naibu Waziri Mkuu kwa ushirikiano mkubwa mlionipa. Watumishi wa ofisi hizi wako tayari kufanya kazi kwa moyo na kukupa ushirikiano ili kuhakikisha kwamba malengo tuliyojiwekea ndani ya serikali yanatekelezwa,” alisema Waziri Mhagama.

Aliongeza kuwa, “Tumefanya kazi usiku na mchana. Kati ya uwekezaji mkubwa ambao umefanywa na Mheshimiwa Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan, ni pamoja na watumishi waliopo kwenye Ofisi hii katika uratibu wa shughuli za serikali.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, alisema kuwa alikabidhi Ofisi hiyo kwa Waziri Mhagama mwaka 2014, na sasa amerudi tena mwaka 2024 baada ya kukaa nje ya Ofisi hiyo kwa miaka tisa. Kabla ya hapo, alishawahi kuitumikia kama Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa miaka tisa.

“Nimeondoka 2014 na sasa nimerudi 2024 kukabidhiwa Ofisi na Waziri niliyemkabidhi wakati huo, ambaye ni Waziri Mhagama. Aidha, nimefanya kazi kwa karibu na Mhe. Mhagama wakati nikiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati Mhe. Mhagama akiwa Katibu wa Chama Bungeni. Ni mapenzi ya Mungu tumekutanishwa tena, watu walewale tunaofahamiana. Nawahakikishia tutaendelea kushirikiana na Katibu Mkuu na watumishi wote ili kuhakikisha tunafanya kazi zetu vizuri,” alisema Waziri Lukuvi.

Awali, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim Yonazi, aliwapongeza Waziri wa Afya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizo.

“Sisi watumishi wenu tunapenda kuwaahidi kwamba tutaendelea kushirikiana nanyi kutekeleza majukumu yetu, lakini pia kuwatumikia wananchi wa Tanzania,” alisema Dk. Yonazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles