Na Mwandishi wetu
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa, amefanya ziara fupi jana Desemba 11,2023 kukagua majaribio ya kichwa cha treni ya umeme ( SGR) kilichopo kwenye Stesheni ya Pugu, jijini Dar es Salaam.
Profesa Mbarawa amesema lengo ni kuona uwezo wa ufanyaji kazi wa kichwa cha umeme cha SGR ambapo hivi sasa kipo kwenye majaribio mbalimbali.
“Majaribio ya kwanza yanafanyika kama majaribio ya mifumo ya breki, mifumo ya breki za umeme na upepo na mwendokasi wa kilomita 160, nimeridhika kwamba kichwa kizuri na kina uwezo mkubwa” amesema Profesa Mbarawa.
Ameeleza kuwa kichwa hicho ni moja kati ya vichwa 17 ambavyo Serikali imenunua kutoka nchini Korea Kusini vyenye thamani ya shilingi bilioni 254 za Kitanzania ambapo vichwa vingine vitatu vinatarajiwa kufika mwishoni mwezi huu.
“Baada ya majaribio haya, majaribio ya pili yanayofuata ni kukifunga kichwa hiki na mabehewa kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, ” amesema.
Aidha Profesa Mbarawa amewasihi wananchi kuendelea kuwa na subira na punde majaribio yatakapokamilika na kujiridhisha, safari za abiria na mizigo zitaanza.