28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI: MARUFUKU KUSOMA HABARI ZOTE ZA MAGAZETI REDIONI

Na Fredrick Katulanda-Mwanza


WAZIRI wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amepiga marufuku vituo vya redio na televisheni kusoma magazeti asubuhi kwa kuwa hatua hiyo inaua soko lake siku hadi siku.

Akizungumza wakati wa kilele chaa Maadhimisho ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ambayo yalifaanyika kitaifa mkoani Mwanza jana, Waziri Mwakyembe alisema kuanzia sasa ni marufuku kwa vituo hivyo kusoma habari zilizoandikwa magazetini na kuelekeza iwapo watapenda kufanya hivyo wasome vichwa vya habari tu.

Alisema magazeti yanafanya biashara japo biashara hiyo ni tofauti na biashara nyingine, hivyo wanaposoma magazeti haya habari zake mpaka zile za ndani kunayafanya kukosa soko na kuyasababishia kushindwa kujiendesha.

“Pengine niseme hapa, kuanzia kesho naomba televisheni na redio ziache kusoma habari zote za magazeti, kama wanataka kusoma basi wasome vichwa vya habari tu, siyo habari yote na mpaka za ndani, mnaharibu biashara za wenzenu,” alisema.

Alisema tafiti zinaonesha usomaji wa magazeti unazidi kupungua duniani, lakini hapa nchini usomaji huo huchangiwa na tabia ya usomaji wa magazeti kwenye redio na televisheni kwa vile wapo watu ambao wamekuwa wakisikiliza habari hizo na kuacha kununua.

Alivionya vyombo vya habari kuzingatia wajibu wao, licha ya kudai uhuru na kubainisha kuwa hakuna uhuru usio kuwa na wajibu na kusema baadhi yake vimekuwa vikiajiri wafanyakazi wanaolipwa kidogo hatua ambayo imekuwa ikisababisha utoaji habari zisizofuata na kuzingatia maadili.

Akizungumzia Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Dk. Mwakyembe alisema anatambua kuwapo manung’uniko ya sheria hiyo.

Alisema atakuatana na wadau wa habari ili kujadiliana maeneo ambayo wanadhani yanahitaji kufanyiwa maboresho.

“Sheria hizi hazikuandikwa katika jiwe, zinaweza kubadilika, leteni maoni yenu na tukae tujadiliane tuone namna tunavyoweza kuzibadilisha,” alisema.

Alisema anajiaandaa kukutana na wadau kwa kuandaa mkutano wa pamoja kwa lengo la kujadiliana na kuwaomba iwapo wanadhani yupo mtu ambaye ana shida na waandishi wamseme ili aelezwe makosa yake na kusameheana.

Hata hivyo, aaliaahidi katika kipindi cha uongozi wake atasimamia uandishi wa habari za uchunguzi na kuzipa msukumo mkubwa, huku akiahidi kukamilisha mchakato wa kanuni za vyombo vya habari kwa mitandao ya kijamii.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), Salome Kitomari alisema siku hii huadhimishwa duniani kwa kutafakari uhuru wa vyombo vya habari na kujieleza kama haki ya msingi ya kibinadamu na kichocheo cha kupata haki nyingine za kiraia.

Alisema takwimu za taasisi kama Reporters Without Boarders (Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka) na Committee to Protect Journalists (Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari – CPJ), zinaonyesha zaidi ya waandishi wa habari 100 wameuawa duniani kote mwaka jana, wakiwa katika harakati za kutimiza majukumu yao.

Alisema kati ya hao, 46 sababu za kuuawa kwao zinajulikana, wengine hazijulikani na kati yao wawili ni wafanyakazi wa kawaida kwenye vyombo vya habari.

“Kwa hapaTanzania, mwaka jana hakuna vifo ilivyoripotiwa. Lakini matukio ya utekwaji nyara na viwango vya unyanyaswaji wa wanahabari vimeongezeka.

“Mwaka jana hapa Tanzania zimeripotiwa kesi za manyanyaso na ukiukwaji wa uhuru wa vyombo vya habari na waandishi wa habari zaidi ya 30. Kesi hizo zinahusisha magazeti kufungiwa, kusimamishwa kwa leseni za Redio na vituo vya televisheni na waandishi kupigwa na kuwekwa rumande kwa mashauri tofauti tofauti ambayo mengi hayakuwa na msingi wa kisheria,” alisemea.

Alitoa mfano wa tukio la kukamatwa kwa mwandishi wa ITV na Radio One mkoani Arusha, Alfani Liundi, kuwapo kwa vitisho vingi vya kuuawa kwa waandishi wa habari kupitia barua pepe na jumbe fupi za simu, lakini hata waandishi kuzuiwa kupata taarifa kwenye baadhi ya ofisi za umma.

Miongoni mwa matukio ya karibuni kabisa ni kushambuliwa na kujeruhiwa takribani wanahabari saba waliokwenda kuripoti habari za kundi mojawapo kati ya mawili yanavutana ndani ya Chama cha Wananchi (CUF).

Kauli mbiu ya mwaka huu ni: Fikra makini katika nyakati Changamoto na Jukumu la vyombo vya habari katika kudumisha amani, usawa na jamii jumuishi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles