Na Editha Karlo, Kigoma
Waziri wa Nishati, January Makamba ametekeleza agizo la makamu wa Rais Dk.Philip Mpango la kufika mkoani Kigoma na kutatua changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara Mkoani humo.
Ziara hiyo ya kikazi ya siku moja Waziri Makamba ilifanyika juzi ambapo alisema kuwa kuna mipango mbalimbali ambayo inalenga kuhakikisha Mkoa wa Kigoma unakuwa na umeme wa uhakika na kutoka kwenye kero ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Alisema katika mipango ya muda mfupi,kituo cha umeme kuzalisha umeme cha Kigoma chenye uwezo wa kuzalisha megawati 6.25 kitaongezewa mashine mbili zitakazo zalisha jumla ya megawati 2.5 kituoni hapo, ambapo mashine ya kwanza yenye uwezo wa megawati 1.25 itakamilika kufungwa Novemba 15, mwaka huu.
Alisema pia miradi ya muda wa kati na mrefy itaunganisha Kigoma na umeme wa gridi na kufanya hali ya kuwepo kwa umeme mwingi na wa bei nafuu kwani kwasasa Kigoma inatumia umeme utokanao na mafuta ambapo hutumia Sh bilioni 3 kwa mwezi kuzalisha nishati hiyo huku mapato yakiwa ni shilingi bilioni 1.5.
Miradi hiyo itakayounganisha Mkoa wa Kigoma na gridi ya Taifa ni ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme itakayotoka Nyakanazi hadi Kakonko pia hadi Kibondo itakayokamilika Machi 2022.
Mradi mwingine ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa KV 132 kutoka Tabora hadi Kigoma ambao unatarajiwa kukamilika Oktoba 2022.
January aliutaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa njia kubwa ya umeme ya msongo wa KV 400 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma ambapo utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka 2023.
Pia kuna mradi mwingine wa umeme unaotarajiwa kuchangia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme kwa Mkoa wa Kigoma ni mradi wa kufua umeme wa maji kutoka mto malagarasi utakaozalisha megawati 49.5 na serikali imeshapata fedha kutoka benki ya maendeo Afrika(AfDB)ba mwakani atatafutwa mkandarasi kwaajili ya ujenzi.
Katika ziara yake hiyo Waziri alikagua mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo Wilayani Kigoma pamoja na Wilayani Kasulu,ambapo Wilaya ya kasulu kuna changamoto ya mitaa mingi kukosa umeme.
“Hapa Kasulu kuna changamoto ya mitaa mingi kukosa umeme ili kutatua tatizo hili utaratibu ndani ya Wizara utafanyika ili kuwezesha TANESCO kupeleka umeme kwenye hiyo mitaa,”alisema Makamba.
Pia Waziri Makama alitembelea kituo cha kuzalisha umeme wa jua cha Nextgen solawazi ambacho kwa sasa kinazalisha umeme wa kiasi cha megawati 1.8 na kupeleka kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha TANESCO, Kampunu hiyo inatarajia kuongeza uzalishaji wa kufikia megawati 4.3 ifikapo tarehe 8 oktoba mwaka huu.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la umeme Tanzania(TANESCO) Maharage Chande alisema kuwa Mkoa wa Kigoma utapata umeme wa gridi ya Taifa ifikapo Machi 2022.