26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Kanyasu apongeza GGML kuchangia maendeleo

Mwandishi Wetu -Geita

MBUNGE wa Geita Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu, amesema hatua kubwa za maendeleo zilizofikiwa hadi sasa katika Halmashauri ya Mji wa Geita zimetokana na mchango mkubwa wa Kampuni ya dhahabu ya Geita Gold Mining (GGM) na mapato yake ya ndani.

Alisema hali hiyo imesababisha Geita kuwa miongoni mwa miji inayokua kwa kasi barani Afrika.

Kanyasu aliyasema hayo alipozungumza na wapigakura wake kuelezea ahadi mbalimbali alizozitekeleza ndani ya miaka minne katika mkutano aliofanya Barabara ya Msalala.

Alisema halmashauri hiyo sasa ina uwezo wa kupanga na kuitekeleza mipango yake ya maendeleo  bila kikwazo chochote kutokana na kuwa na nguvu ya fedha.

“Licha ya kasoro nyingi za GGML, huwezi kusema maendeleo ya Geita mjini yaliyofikiwa kwa sasa pasipo kuwataja,” alisema.

Kanyasu alisema mgodi huo umetoa mchango mkubwa katika ujenzi wa Shule ya Wasichana Nyankumbu ambayo ni moja ya shule inayofanya vizuri kidato cha nne na kidato cha sita mkoani hapo.

Alisema mbali na hiyo, mgodi huo umetoa mchango mkubwa kupitia fedha za ujirani mwema kwa kujenga madarasa 120, shule za msingi sita  na shule ya kidato cha tano iliyojengwa Kata ya Kasamwa.

Akizungumza kuhusu suala la mikopo, Kanyasu alisema hadi hivi sasa halmashauri hiyo imetoa mkopo wa Sh bilioni 1.7 kwa wanawake, walemavu na vijana.

“Tumewakopesha  ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuingia kwenye biashara mbalimbali,” alisema.

Kuhusu afya, Kanyasu alisema wamefanikiwa kujenga vituo sita, mbali na hospitali ya mkoa ambayo inaendelea kujengwa.

Alisema mgodi huo umetoa mchango mkubwa wa ujenzi wa soko la madini, ambalo tangu kukamilika kwake na kuanza kufanya kazi, halmashauri imekuwa na uwezo wa kukusanya  Sh milioni 5 kila siku.

Kuhusu maji, Kanyasu alisema halmashauri imepata Sh bilioni 100 kwa ujenzi wa mradi wa maji utakaokuwa na uwezo wa kuwahudumia wakazi wote wa mji huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles