ROME, ITALIA
MZOZO wa kidiplomasia unazidi kufukuta kati ya wanachama wawili waanzilishi wa Umoja wa Ulaya, Italia na Ufaransa baada ya mmoja wa mawaziri wa Italia kutoa mwito kwa Wafaransa kumng’oa Rais Emmanuel Macron.
Hiyo inakuja siku moja tu baada ya Naibu Waziri Mkuu wa Italia,Luigi Di Maio kutaka Ufaransa iadhibiwe kwa kutumia sera za kikoloni barani Afrika kuwatia ufukara Waafrika na kuwafanya wakimbilie Ulaya.
Juzi Waziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Matteo Salvini, alitumia ukurasa wake wa Facebook kumshambulia vikali Rais Macron akimuita rais mbaya anayependa maneno lakini kuliko vitendo.
Salvini anayeongoza chama kinachopinga wahamiaji, amemtuhumu Macron kwa kuipa darasa Italia na kumtaka badala yake awaruhusu wahamiaji walioko mpakani mwa nchi yake na Ufaransa.
“Ikiwa kweli Macron ni mzuri anaweza kuthibitisha kwa kuwaruhusu maelfu ya wakimbizi waliopo Italia na ambao aliwaahidi ukarimu pamoja na mataifa mengine ya Ulaya.
Si suala la Matteo Salvini kuingilia siasa za Ufaransa, lakini natarajia wananchi wa Ufaransa hapo Mei 26 watamchagua mtu mwingine anayewawakilisha zaidi, aliye makini zaidi, aliye wa matendo zaidi. Namfikiria mtu kama Marine Le Pen.”, alisema Salvini.
Lakini akimjibu Salvini, waziri anayeshughulikia masuala ya Ulaya katika Serikali ya Ufaransa, Nathalie Loiseau, alisema Wafaransa walikuwa na muda wa kuchagua baina ya Le Pen na Macron na wakafanya chaguo lao.
Akitumia mtandao wako wa Twitter, Loiseau aliandika: “Matteo Salvini anawatukana Wafaransa. Wataliano wanafaidika nini? Hawafaidiki kitu. Je, matusi haya yanabadili kitu kwenye siasa za Ufaransa? Hapana!”
Wakati serikali ya Italia ikikabiliwa na lawama kwa vifo vya wahamiaji kadhaa vilivyotokea hivi karibuni kwenye Bahari ya Mediterania, Naibu Waziri Mkuu Luigi Di Maio alijaribu kuzihamishia lawama hizo kwa Ufaransa kuwa ni chanzo cha wahamiahji wa Afrika kukimbilia Ulaya.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa ilimuita balozi wa Italia siku ya Jumatatu kutokana na kauli hiyo.
Vuguvugu la Nyota Tano la Di Maio linaunga mkono vuguvugu la Vizibao Manjano nchini Ufaransa linaloipinga Serikali ya Rais Macron.