26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Waziri Gwajima awageukia wanaume kuhusu ukeketaji

Mwandishi Wetu, Tarime

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, amesema  vitendo vya ukeketaji unaendelea kwa sababu wanaume hawajaamua kusema ukeketaji basi.

Dk. Gwajima amesema vitendo hivyo vinaweza kukomeshwa endapo wanaume watakaa katika makundi yao na kujadiliana jinsi ya kuvikomesha.

Amesema wakati umefika kwa jamii kuachana na visingizio vinavyosababisha kuendelea kwa vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto na badala yake kusimamia misingi ya upatikanaji wa haki.

Waziri Gwajima amesema hayo wilayani Tarime mkoani Mara alipotembelea kituo Nyumba Salama cha Masanga kinachotumika kuwalea watoto waliokumbwa na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia au walio katika hatari ya kukumbwa na vitendo hivyo.

“Jamii lazima ishiriki kikamilifu kufuatilia matatizo yanayowakumba wanajamii husika na kama wanashindwa kufanya hivyo wanakuwa wanahusika kwa namna moja au nyingine na vitendo hivyo,” amesema Gwajima.

 Amesema baadhi ya maeneo nchini watoto wanafanyiwa vitendo vya kikatili na kukoseshwa haki ya elimu wakati watumishi wanaopaswa kuingilia kati suala hilo wanabaki kimya na kuongeza kuwa baadhi ya watendaji katika ngazi mbalimbali wanabweteka na kulipwa mshahara bila kuufanyia kazi.

Wakati huo huo Dk. Gwajima ametuma salamu kwa watendaji wa moja ya mtaa na Kata mkoani Mwanza ambao aliishi mtoto mmoja aliyekoseshwa haki ya kwenda shule ili abaki nyumbani akimuuguza bibi yake.

“Mwanza mwambieni, Mtendaji wa Mtaa, Kata, ambayo yupo mtoto aliyenyimwa haki ya kwenda shule, ana miaka tisa pamoja na akili yote hiyo haendi shule na watendaji wametulia wanasubiri ndugu wajitokeze nakuja Mwanza,” amesisitiza  Dk. Gwajima

Akisoma  taarifa ya Kituo cha Masanga  kwa Waziri, Meneja wa Mradi wa kupinga ukeketaji kituoni hapo, Valerian Mgani, amesema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto ya bweni, chombo cha usafiri na watoto wa kike kukatishwa masomo, kukeketwa na kuozeshwa katika umri mdogo.

Ameongeza kuwa Kituo cha Nyumba Salama cha Masanga kilianzishwa na mwaka 2006 na kusajili mwaka 2015 kwa lengo la kuwahudumia watoto wahanga wa ukatili ukiwemo ukeketaji ambapo hadi sasa kituo hicho kinahudumia walengwa 34 kati yao mmoja wa kiume.

Katika hatua nyingine, Dk. Gwajima alitembelea Makao ya Watoto ya City of Hope yaliyoko katika shule ya Kumbukumbu ya Dk. John Chacha inayojishughulisha na huduma kwa jamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles