Na Brighter Masaki, Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amewaagiza TCRA kuzifungulia Online TV zote ambazo zilifungiwa, huu ukiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, alilolitoa hapo juzi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo Aprili 8, Bashungwa amesema hadi sasa kuna TV Mtandao 440 ambazo zimesajiliwa.
“Mpaka sasa tuna TV za Mtandaoni (Online TV) 440 ambazo tumezisajili, kwa kushirikiana na Waziri mwenzangu wa Mawasiliano (Dk. Faustine Ndugulile) nimetoa maelekezo Online TV zote ambazo zilizuiwa zianze kufanya kazi lakini ni kwa kufuata masharti kama ya usajili,”amesema Bashungwa.
Itakumbukwa Aprili 6, Mwaka huu Rais Samia Suluhu baada ya kuwaapisha Viongozi Wapya Ikulu Dar es salaam alisema; “Wizara ya Habari, nasikia kuna Vyombo vya Habari mmevifungia, sijui Viji- TV vya mikononi vile, vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali, tusiwape mdomo wa kusema tunabinya Uhuru wa Vyombo vya Habari, tusifungie tu kibabe,”alisema Rais Samia.
Pia ameongeza kuwa kuhusiana na magazeti yaliofungiwa ni suala jingine nakwamba milango ipo wazi kwa wahusika kufika ofisini kwa mazungumzo ili kujua namna ya kutatua.