27.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Bashe ahaidi kutatua changamoto wakulima wa miwa

Na Asha Bani, Mtanzania Digital

KAMPUNI ya Sukari ya Kilombero (KSCL) imeanza kuwaunganisha wakulima na taasisi mbalimbali ili kuwapatia elimu na msaada katika kuboresha mbinu zao za kilimo na kukuza stadi za biashara.

Kampuni hiyo pia imefanya maboresho katika Idara yake ya Huduma kwa Wakulima na kuongeza idadi ya wafanyakazi wa huduma kwa wakulima kutoka wafanyakazi nane hadi 48.

Pia KSCL itashikrikia na Mfuko wa Maendeleo wa Tasnia ya Sukari (SIDTF) na Taasisi ya Sukari ya Taifa (NSI) na wadau wengine kuandaa programu za maendeleo ya Wakulima.

Hayo yamesemwa jana Jijini Morogoro na Ephraim Mafuru, Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano wa KSCL, wakati akimueleza waziri wa Kilimo Hussein Bashe kuhusu hatua mbali mbali zinazochukuliwa na kampuni hiyo katika kuboresha kilimo cha miwa kwa wakulima wenye mktaba wa ugavi.

Mafuru alisema kuwa pia KSCL imeanza taratibu za mazungumzo na wakulima wa miwa ili kuingia makubaliano ya manunuzi ya pamoja ya pembejeo kati ya kampuni hiyo na wakulima, hali itakayowasaidia wakulima kupata pembejeo za kilimo kwa wakati unaostahili.

“Mkataba huo utaainisha muundo wa upatikanaji wa gharama za mtaji na mabohari kulingana na miongozo kutoka mamlaka husika,” alisema Mafuru.

Kampuni ya Sukari ya Kilombero imefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 166 katika biashara katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Uwekezaji huo umehusisha uboreshaji wa uzalishaji wa miwa na sukari pamoja na uwekezaji katika kiwanda cha kisasa chenye uwezo wa kusambaza Kilolita milioni 12 za pombe yenye ubora wa juu.

Illovo Sugar Africa, inamilikiwa na Kampuni ya British Foods ya Nchini Uingereza kwa asilimia 75 ya mtaji wa hisa uliotolewa kwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, na kiasi cha asilimia 25 cha hisa zinamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.

Waziri wa Kilimo,  Hussein Bashe ambaye alifanya mkutano wa hadhara na wakulima wa nje wa miwa Kilombero ili kusikiliza changamoto zao katika azma ya kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo cha miwa, amesema kuwa serikali itatengeneza miundombinu ya umwagiliaji na kuunda tume maalum ya kusimamia kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo ofisi za umwagiliaji za halmashauri zitasimamia uendelevu wa miundombinu hiyo.

Bashe alisema kuea Tume ya Umwagiliaji itafanya kazi na KSCL katika kuandaa mpango mkuu wa umwagiliaji kwa ajili ya KSCL na Wakulima kabla ya kuwakilisha mpango huo katika Wizara ya Kilimo.

Alisea kuwa kufuatia changamoto za upatikanaji wa mbolea uliopelekea kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo, serikali inaendelea na mpango wa kuanzisha ruzuku ya mbolea kwa wakulima wote nchini ambayo itawanufaisha wakulima hao na kupunguza changamoto iliyopo ya ongezeko la bei.

Akijibu hoja ya upatikana mbegu bora kutoka kwa wakulima hao, Bashe aliahidi kuwa serikali itaendesha kitalu cha kuzalishia mbegu ambapo wakulima watapata mbegu bora kutoka serikalini. Kampuni ya Sukari ya Kilombero ilikubali kutoa ardhi ya hekari 400 kuiwezesha serikali kuendesha mradi huo wa uzalishaji mbegu.

“Ubora wa muwa ni mchakato kuanzia mbegu iliyopandwa, namna ulivyolima, namna ulivyovuna na namna unavyopeleka kiwandani. Nimesikia kilio cha upatikanaji wa mbegu, tunaanzisha kitalu cha hekta 400 cha serikali cha uzalishaji wa mbegu hapa kwenu,” alisema Bashe.

Licha ya wakulima wa Kilombero kuwa ndio wakulima wanaolipwa fedha nyingi zaidi (kwa tani) nchini Tanzania, Waziri alisema upo uwezekano wa kuboresha kiwango chao cha malipo na kuitaka Kampuni ya Kilombero na wakulima kukaa na kupitia upya mkataba wa ugavi ili kuona maeneo yanayoweza kuwaongezea wakulima mapato na pia kuimarisha uwazi katika mfumo wao wa mgawanyo wa mapato.

“Nitaunda timu itakayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ili kuangalia mchakato wa maboresho ya mkataba wa ugavi na kuwahusisha wakulima ili kujianda na upanuzi wa kiwanda,” alisema.

Waziri aliipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wadau kwa kuwezesha usajili wa wakulima wapya 2,000 katika kanzi data ya kidijitali na kufanya jumla ya wakulima waliosajiliwa kufikia 9,700. Hatua hiyo itaiwezesha serikali na mamlaka husika kufuatilia maendeleo ya wakulima ili kuwapatia misaada mbalimbali.

“Kwenye mazao ya korosho, pamba na kwenye tumbaku mkulima hatakiwi kuwa na fedha taslimu ili kununua pembejeo kwa vile tayari ana soko. Tunahitaji kujua aina na mahitaji ya mbolea na viuatilifu. Kupitia usajili wa wakulima, mabenki yatatoa fedha na mkulima atakatwa atakapouza mazao yake,”alisema Bashe.

Kuhusu upatikanaji wa mitaji, Waziri aliziagiza mamlaka husika kuhakikisha kuwa wakulima wote wanasajiliwa katika kanzi data ya kidijitali ili kuongeza imani kwa taasisi za kifedha na kukuza upatikanaji wa mikopo kwa wakulima.

Pia alizitaka taasisi za fedha kupitia upya masharti yao ya mikopo ili kuwawezesha wakulima wadogo kupata mikopo. KSCL iliahidi kufanya kazi na wakulima hao pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ili kuvutia fursa za mitaji kwa wakulima.

Bashe pia alisema serikali itashirikiana kwa karibu na Kampuni ya Sukari ya Kilombero katika kutengeneza mfumo utakaohakikisha uwazi kwenye vipimo vya ubora wa miwa ili kuwahakikishia wakulima kuwa wanalipwa kiasi stahiki kulingana na kiwango cha sukari kwenye miwa yao. Serikali itaunda kikosi kitakachofanya kazi na KSCL na kuripoti matokeo ya vipimo vya ubora wa miwa kwa wakulima hao wa nje.

Waziri alimuagiza mrajisi wa vyama vya ushirika kusimamia kwa ukaribu shughuli za vyama vya ushirika ikiwemo katiba zao, uteuzi wa viongozi, utoaji wa zabuni, malipo kwa viongozi wa vyama ili kuhakikisha haki za wanachama zinalindwa.

Kampuni ya Sukari ya Kilombero inafanya shughuli za uzalishaji wa sukari katika Mkoa wa Morogoro na inajumuisha maeneo mawili ya kilimo na viwanda vya sukari ambayo ni Msolwa na Ruembe. Kampuni inazalisha sukari chini ya chapa maarufu ya ‘Bwana Sukari’.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles